Na Mwandishi Wetu, Dar
NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar amezindua rasmi Mpango wa Utekelezaji Mwongozo wa kuwarejesha shule wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanatimiza ndoto na malengo yao kwenye elimu.
Dkt. Omar amefanya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam huku akibainisha kuwa Mpango huo muhimu utatoa dira kwa Serikali na wadau wa elimu katika kutekeleza kikamilifu sera ya elimu na Mwongozo wa urejeshaji ili kuhakikisha watoto wote, bila kujali changamoto walizokutana nazo, wanapata nafasi ya kuendelea na masomo na kutimiza malengo yao.
"Watoto wetu wa kike na wa kiume, wanapokatisha masomo, si mwisho wa maisha yao, kuna fursa zaidi ya elimu ili kufikia malengo yao na waweze changia maendeleo ya taifa kwa ujumla," amesisitiza Dkt. Omar.
Aidha ameupongeza Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo unaolenga kutoa fursa sawa kwa watoto wote katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari.
Katika hatua ingine Dr Omar pia amezindua taarifa ya utafiti uliofanyika juu ya utekelezaji Mwongozo wa urejeaki kwa kundi moja wa wanafunzi wa kike waliokatisha masomo kutokana na ujaouzito.
Taarifa hiyo inaelezea mafanikio makubwa ambayo yamewezesha wanafunzi wa kike zaidi 13,000 na wa kiume 17,000 kurejea kuendelea na masomo.
Awali akizungumza Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Kitaifa, Bi. Martha Makala alisema mpango huo ulioandaliwa na Tenment kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na taasisi ya Elimu ya Watu Wazima utasaidia kutumia rasilimali kwa ufanisi, kuboresha ubora wa kazi.
Mpango huu pia utasaidia kuhakikisha kila mwanafunzi anayekatiza masomo kwa sababu mbalimbali anaendelea kupata fursa ya kurejea shuleni, huku changamoto za kijamii, kifamilia na kiuchumi zikitatuliwa kwa njia shirikishi na endelevu.
"...Ni matumaini yetu kuwa kupitia mpango huu Serikali, wadau wa maendeleo, na mashirika ya kiraia tutaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kuhakikisha kila mtota anapata fursa sawa ya kielimu, bila vikwazo vyovyote," alisema Bi. Makala.
Pamoja na hayo aliiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuendelea kuboresha mfumo wa tahadhari ya mapema kuhusu uachaji wa masomo ili kudhibiti hali hiyo kabla ya kutokea na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali.
Hata hivyo, Bi. Makala aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Jukwaa la Kitaifa la Utetezi wa Elimu kwa Mtoto wa Kike ambao kwa pamoja wanapigania elimu jumuishi, inayozingatia usawa wa kijinsia.
| Sehemu ya wanafunzi walioshiriki katika uzinduzi huo. |

No comments:
Post a Comment