Na Mwandishi Wetu, Dar
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua huduma mpya ya mawasiliano ijulikanayo kama T-Fibre Triple Hub, inayompa uhuru zaidi mteja wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako kupata vitu vitatu kwa wakati mmoja na popote alipo.
Katika huduma hiyo mteja akijiunga na T-Fibre Triple Hub anapata huduma ya intaneti ya kasi nyumbani na hata eneo lingine popote nje ya nyumbani, anapata huduma ya muda wa maongezi popote na pia huduma ya sms popote pale alipo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Meneja Biashara na Promosheni wa TTCL, Bi. Janeth Maeda, alisema huduma hiyo ni ubunifu unaolenga kumrahisishia mteja kupata huduma tatu muhimu za mawasiliano katika kifurushi kimoja yaani intaneti ya kasi, simu ya mezani na huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi.
Aliongeza kuwa ubunifu huo ni juhudi za TTCL kuiunga mkono Serikali katika kukuza uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), jambo ambalo linaleta chachu ya maendeleo kutokana na ulazima wa huduma za TEHAMA kwa sasa.
“Kupitia T-Fibre Triple Hub, wateja wetu wataweza kupata huduma zote muhimu kwa pamoja bila usumbufu wa kulipia huduma tofauti lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata mawasiliano ya uhakika, nafuu na yenye kasi zaidi,” amesema Bi. Maeda akizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa huduma hiyo.
Amebainisha kuwa TTCL inaendelea kutekeleza mikakati ya kuunga mkono sera za Serikali katika kukuza uchumi wa kidijitali, hususan katika nyanja za elimu, biashara na huduma za kijamii.
“Serikali imesisitiza umuhimu wa matumizi ya TEHAMA katika kuleta maendeleo. Sisi kama TTCL tumejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, hata aliye kijijini, anapata huduma hizi kwa urahisi,” amesisitiza.
Aidha, TTCL imesema huduma ya T-Fibre Triple Hub inatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi katika sekta mbalimbali kwa kurahisisha upatikanaji wa intaneti ya kasi, sambamba na kuongeza ufanisi katika biashara na taasisi za umma.
Kwa mujibu wa shirika hilo kubwa la mawasiliano nchini, huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za kuendelea kujitanua hadi maeneo ya vijijini na pembezoni, ambako upatikanaji wa mawasiliano ya kisasa umekuwa changamoto kwa wananchi.

No comments:
Post a Comment