HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 21, 2025

MAUZO YA SAMAKI YAPAA NJE YA NCHI

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, Novemba 21, 2025, alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach kwa lengo la kuhamasisha dhana ya Uchumi wa Buluu, ulaji wa samaki na mazao yake, pamoja na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa mazingira na rasilimali za uvuvi yaliyofanyika kwa muda wa siku 2 kuanzia tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025.

Akizungumza wakati wa hotuba yake, Bi. Meena alisema kuwa uuzaji wa samaki nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 42,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 509.9 hadi tani 59,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 755. Sambamba na hilo, idadi ya wavuvi imeongezeka kutoka 198,475 mwaka 2023 hadi 201,661 mwaka 2024. Idadi ya viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nayo imeongezeka kutoka 21 hadi 64 katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024.

“Sisi sote tunafahamu kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za maji ikiwemo bahari, mito, mabwawa, maziwa na maeneo oevu, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa buluu. Watanzania wapatao milioni sita wanategemea shughuli za uvuvi katika kujipatia kipato. Tukizingatia kuwa nchi ina jumla ya takribani watu milioni 62 hadi 63, ina maana kuwa asilimia 10 ya Watanzania wanategemea sekta hii—jambo linaloonyesha umuhimu wake kwa uchumi wa taifa.”

“Serikali itaendelea kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, ufugaji wa samaki kwa njia za vizimba na mabwawa, pamoja na kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki, kupunguza uharibifu wa mazingira, kuzuia uvamizi wa fukwe na kupunguza shinikizo la uvuvi,” alisema Bi. Meena.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi ili kuimarisha usalama wa chakula, lishe, kipato cha kaya na uchumi wa taifa. Kutokana na juhudi hizo, tumeshuhudia ongezeko la uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 479,976 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 hadi tani 522,788 zenye thamani ya shilingi trilioni 4.3 mwaka 2024.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Emelda Teikwa, amesema kuwa wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamefanya maadhimisho haya katika mkoa wa Dar es Salaam na Rukwa. Ameongeza kuwa Siku ya Mvuvi Duniani imekuwa ikitumika kama jukwaa la kujenga uelewa kwa wavuvi na kuelimisha kuhusu uhifadhi wa mazingira na usafi wa fukwe, na pia kuelimisha kuhusu uvuvi endelevu.

Bi. Teikwa aliongeza kuwa katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu, wizara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya jamii.

Akitoa salamu kwa niaba ya wavuvi, Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) eneo la Kawe Beach, Bw. Mudu Mohamed, ameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti uvamizi wa fukwe ambao umeanza kukithiri katika maeneo ya Kawe, Kunduchi, Msasani, Mbweni na Ununio.

Bw. Mudu amesema uvamizi huo unaathiri shughuli za uvuvi na kuhatarisha ustahimilivu wa mazingira sambamba na kuhatarisha fursa za kibiashara kwa akina mama na vijana wanaotegemea fukwe hizo. Ameomba Serikali kuhakikisha suala hilo linasimamiwa kwa umakini na haraka, sambamba na kuwaongezea BMU boti moja ya uvuvi itakayosaidia kufanikisha doria, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za bahari na kulinda mazingira ya fukwe.

Katika siku ya kwanza ya maadhimisho (20 Novemba 2025), shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo kampeni za uhifadhi wa mazingira, kufanya usafi wa fukwe, midahalo iliyowawezesha wavuvi kupata elimu na kuuliza maswali mbalimbali, pamoja na uhamasishaji wa ulaji wa samaki kwa manufaa ya afya na uchumi.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu amezindua mpango wa kitaifa wa usimamizi wa samaki aina ya Jodari na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa, pamoja na kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho kujionea bidhaa za mazao ya uvuvi.

Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo “Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Endelevu: Msingi Imara wa Uchumi wa Buluu.”
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, akiongea na wadau wa Uvuvi na Mazingira Novemba 21, 2025 alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (katikati) akizindua mpango wa kitaifa wa usimamizi wa samaki aina ya Jodari na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa Novemba 21, 2025 alipokuwa akihitimisha kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.





Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena akitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho ya bidhaa mbalimbali za mazao ya Uvuvi yanayotengenezwa na wajasiliamali Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) eneo la Kawe Beach, Bw. Mudu Mohamed akisoma risala kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.
Wadau mbalimbali wa Uvuvi na Mazingira wakisikiliza hutuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena (hayupo pichani) Novemba 21, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyoanza  tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025 Jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad