Na Mwandishi Wetu
HOSPITALI ya Shifaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imezindua kitengo maalum kwa ajili ya matibabu ya wenye maradhi ya kisukari.
Uzinduzi wa huduma hizo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa taasisi binafsi.
Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk Emmanuel Maganga alisema jana kuwa kitengo hicho chenye wataalamu bobezi wa maradhi hayo kitasaidia kupunguza tatizo la ugonjwa huo ambao unaonekana kuendelea kukua kwa kasi nchini.
Alisema ongezeko la wagonjwa wa kisukari nchini ndio uliosababisha uongozi wa hospitali hiyo kuona umuhimu wa kuanzisha kitengo hicho kama njia ya kupunguza tatizo hilo.
“Miongoni mwa magonjwa yanayosumbua sana kwa sasa hapa nchini ni kisukari ukiangalia miaka ya nyuma utafiti ulionyesha kuwa Dar es Salaam ilikuwa na wagonjwa wasiozidi 600,000 wa kisukari lakini kwa utafiti wa mwaka jana ulionyesha kuwa wagonjwa wa kisukari wamefikia 3,000,000,” alisema
“Kwa hiyo unaona kabisa ugonjwa wa kisukari unaendelea kukua kwa kasi ya kutisha na unaenda sanjari na ugonjwa wa figo kwa maana kwamba sababu kubwa ya matatizo ya figo kote duniani huwa ni kisukari kwa hiyo ukipambana na kisukari umepambana na ugonjwa wa figo,” alisema Dk Maganga
Alisema asilimia 50 ya fedha zinazolipwa kwa matibabu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), zinalipia magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiongozwa na maradhi ya figo na kisukari.
“Ndiyo maana Shifaa ikaona iwe na kitengo ambacho mgonjwa akija ndani ya saa moja ataonwa na daktari bingwa wa kisukari, daktari bingwa wa magonjwa ya macho na wataalamu wa lishe bora na haya yote atayapata sehemu moja tu,” alisema Dk Maganga
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Gunini Kamba alisema serikali imefurahi kuona Shifaa inaanzisha kitengo hicho kwani kinasaidia jitihada za serikali kupunguza magonjwa.
Kamba ambaye ni mratibu wa ushirikiano baiona ya serikali na sekta binafsi mkoani Dar es Salaam alisema serikali inafurahia ushirikiano uliopo baina yake na sekta binafsi kwenye sekta ya afya kwa kuwa wanasaidia jitihada ambazo zinafanywa na serikali kupambana na magonjwa.
“Kwa sasa nchi yetu inahamasisha utalii tiba kwa hiyo ukiona hospitali ilivyojengwa kwa ubora wa hali ya juu kama huu lazima tufurahie, hii hospitali haina tofauti na hospitali zilizoko kwenye mataifa yaliyoendelea kwa hiyo hatua kama hii sisi serikali tunaipongeza sana,” alisema
“Hata kwenye dira ya 2050 ushirikiano wa sekta binafsi na umma kwenye sekta ya afya umetajwa kwa hiyo tutahakikisha tunadumisha huu ushirikiano ili watanzania waendelee kunufaika na huduma za afya,” alisema
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hospitali BInafsi, Dk Egina Makwabe, alisema hospitali ya Shifaa ni kubwa kuliko zote nchini nan i ya kwanza kwa Afrika Mashariki kutokana na kujengwa kwa viwango vya kimataifa.
“ Mimi mwenyekiti nafurahi kuona mwanachama wangu anazindua kitengo muhimu kama hiki ambacho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na wageni kutoka nje, hili ni jambo la kujivunia na nawashauri watanzania watumie fursa hii kupambana na ugonjwa wa kisukari,” alisema
Sunday, November 16, 2025
Home
Unlabelled
HOSPITALI YA SHIFAA YAANZISHA KITENGO MAALUM CHA MATIBABU YA KISUKARI
HOSPITALI YA SHIFAA YAANZISHA KITENGO MAALUM CHA MATIBABU YA KISUKARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)








No comments:
Post a Comment