TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH) imewatembelea wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbwenitete jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Sayansi Duniani, kwa lengo la kuwahamasisha vijana hao kujikita katika ubunifu na matumizi ya sayansi katika kutatua changamoto za kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 10, 2025, Mratibu Mkuu wa Tafiti na Bunifu kutoka COSTECH, Dkt. Prosper Masawe, amesema amevutiwa na ubunifu mbalimbali uliooneshwa na wanafunzi wa shule hiyo, ambao unaonesha uwezo mkubwa wa kubuni suluhu za changamoto katika jamii.
“Tumeshuhudia bunifu nyingi zenye manufaa kwa jamii. Tunawataka wanafunzi hawa kuwasilisha kazi zao COSTECH kupitia mfumo wa Walk in Innovator ili tuweze kuzitambua, kuziweka kwenye kanzidata na kuwaunganisha na wadau pale watakapohitajika,” amesema Dkt. Masawe.
Ameongeza kuwa COSTECH pia imewafundisha wanafunzi hao kutumia mfumo wa “MAKISATU” ambao utawasaidia kushiriki katika jukwaa la bunifu za ushindani litakalotangazwa hivi karibuni kupitia tovuti ya COSTECH.
Kwa upande wake, Mwalimu Isack Exaud Zacharia, amesema shule ya Mbwenitete imekuwa kitovu cha kuibua vipaji vipya vya sayansi nchini, huku maadhimisho hayo yakichochea zaidi hamasa ya kujifunza kwa vitendo.
“Masomo ya sayansi yanahitaji hamasa. Sisi tunasisitiza kujifunza kwa vitendo, jambo linalowafanya wanafunzi kupenda sayansi. Hata hivyo, bado tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya maabara ili kukamilisha mazingira ya kujifunzia kwa ufanisi,” ameongeza.
Nao wanafunzi wa shule hiyo wameipongeza COSTECH kwa kuweza kufika katika shule hiyo na kuwaeleza majukumu makubwa ambayo wanayafanya na kuwapa fursa ya kupeleka bunifu zao ziweze kutambulika na hata baadaye ziweze kutumika katika kutatua changamoto kwenye jamii.
"Tumepata fursa kuifahamu COSTECH, hii imetufanya kupata fursa ya kuona umuhimu wa kuendelea kuwa wabunifu ili tuweze kuwasilisha COSTECH waweze kutushauri na kuboresha bunifu zetu ambazo zitakwenda kusaidia kutatua changamoto kwenye jamii zetu" amesema Good Bernard, mwanafunzi wa shule hiyo,












































































No comments:
Post a Comment