HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 8, 2025

Ziara ya OCPD Uingereza yatoa mafunzo ya kidigitali ya sheria

 

 

 Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Waandishi wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wamefanya ziara ya mafunzo nchini Uingereza, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika Mkutano wa Jumuiya ya Waandishi wa Sheria wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Association of Legislative Counsel – CALC), Kanda ya Ulaya.

Maafisa kutoka OCPD wakiongozwa na Kaimu  Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo wa OCPD, Bi. Rehema Katuga(wa Pili kutoka kulia), Bwana Bavoo Junus, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora (wa kwanza kulia), Bw. Shabani Kabunga ambye ni Kaimu Mkurugenzi msaidiazi Divisheni ya Uandishi wa Sheria(wa pili kutoka  kushoto  pamoja na Bw. Alfred Nyaronga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wakiwa kwenye picha ya pamoja ndani ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Uingereza.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo wa OCPD, Bi. Rehema Katuga, amesema safari hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imewapa fursa ya kuona kwa vitendo namna wenzao wa Uingereza wanavyotekeleza majukumu yao katika nyanja ya uandishi wa sheria kwa kutumia mifumo ya kisasa na mipango madhubuti ya mafunzo.

“Tulipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza inayojulikana kama Office of Parliamentary Counsel (OPC), ambapo tulijifunza kwa kina jinsi wanavyofanya kazi kama taasisi huru inayojitegemea lakini yenye uhusiano wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hii imetupa mwanga juu ya namna tunavyoweza kuboresha mifumo yetu nchini,” alisema Bi. Katuga.

Aidha Katuga amesema kupitia ziara hiyo, maafisa hao waliweza kujifunza pia kuhusu namna nchi hizo zinavyoshughulikia masuala ya urekebu wa sheria na jinsi mifumo yao ya utunzaji wa kumbukumbu inavyowezesha urahisi wa kupata taarifa za kisheria kwa wananchi.

“Tunarejea nchini tukiwa na maono mapya, tumepata somo la namna tunavyoweza kuboresha Ofisi yetu kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia, kubuni mpango wa mafunzo endelevu kwa waandishi wa sheria, na kuhakikisha kuwa taratibu zote za uandishi wa sheria zinakuwa wazi, shirikishi na zenye ufanisi,” alihitimisha Bi. Katuga.

Bi. Katuga amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa OCPD wa kuboresha utendaji wake kupitia mafunzo ya kimataifa, ubadilishanaji wa uzoefu, na ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika nyanja ya uandishi wa sheria na urekebu wa sheria imelenga kujifunza mbinu, mifumo na teknolojia mpya za uandishi na urekebu wa sheria ili kuboresha utendaji wa ofisi hiyo muhimu nchini Tanzania.

Nae Bw. Alfred Nyaronga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema timu hiyo pia ilitembelea Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka (The National Archives) ambako walijifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker, unaotumika katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria nchini Uingereza.

Amesema mfumo wa Lawmaker ni wa kipekee unawawezesha wadau wote wa uandishi wa sheria kuanzia wizara, bunge, ofisi ya mwandishi wa sheria, hadi mpigachapa wa serikali  kufanya kazi kwa pamoja katika jukwaa moja la kidigitali ambapo mswada unaweza kupitiwa, kurekebishwa, na kupitishwa hatua kwa hatua ndani ya mfumo huo hadi unapokuwa sheria kamili.

Bwana Nyaronga ameongeza kuwa mfumo huo pia hutumika katika urekebu wa sheria (consolidation of laws) kwa kuruhusu sheria zilizofanyiwa marekebisho kuunganishwa moja kwa moja, hivyo kumwezesha mwananchi au mdau yeyote kupata toleo la kisasa la sheria husika mara moja na hivyo kunaongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa taarifa za kisheria kwa umma, jambo ambalo tungependa kuona linatekelezwa pia hapa nchini.

“Kwakweli huo ni mfumo mzuri ambao umeleta mapinduzi makubwa kwenye masuala ya uandishi wa sheria nchini Uingereza nasi tunashawishika kuiona umuhimu wa ofisi yetu kuanza mazungumzo nao maana wameonesha utayari wa kutujengea uwezo watu wetu kisha tuweze kuuleta hapa nchini ili na sisi tutoke kwenye matumizi ya karatasi tuingie kwenye mfumo huu wa uandishi wa sheria kidigital” Alisema Nyaronga.

Kwa upande wake Bwana Bavoo Junus, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora kutoka OCPD amesema kuwa pamoja na nchi za magharibi kupiga hatua kubwa kwenye matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria lakini pia wameweza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoletwa na matumizi ya mifumo hiyo na kuongeza ufanisi.

Aidha Junus amesema jambo lingine muhimu ambalo wamejifunza kwenye ziara hiyo ambalo wanalipa kipaumbele walipoonana na Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza, anayejulikana kama First Parliamentary Counsel, pamoja na Second Parliamentary Counsel ni mafunzo kuhusu jinsi wanavyosimamia shughuli za uandishi wa sheria na kuwajengea uwezo waandishi wapya kupitia mafunzo ya ndani (in-house training).

“Wenzetu wameweka utaratibu wa kuwa na mafunzo ya ndani ili kusaidia Waandishi wachanga na wageni kwenye fani hiyo, ambapo waandishi wa sheria wenye uzoefu (senior drafters) hupewa wajibu wa kuwafundisha waandishi wapya kwa kipindi cha mwaka au zaidi hivyo mfumo huu wa ushauri na mafunzo ya vitendo umekuwa na matokeo makubwa katika kukuza ujuzi na kuimarisha ubora wa kazi, ingawa pia ni jambo ambalo OCPD imeshaanza kulitekeleza na tunatamani liwe endelevu,” alisema Bwana Junus.

 Aliongeza” Jambo lingine tulilojifunza, wenzetu kwenye Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza ofisi yao wameigawanya katika timu nne na kila timu ina kiongozi wake na inafanya jambo mahususi ya kuyashughulikia kwenye sekta fulani na hivyo kuwa na ushiriki wa jumla katika eneo husika na sio mtu mmoja kuwa na taarifa fulani pake yake na akikosekana kazi zinasimama, hii inawezesha wote kuelewa kila jambo kwa undani na kazi kutokwama na kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa wote”.

Wataalamu hao kutoka Tazania walipata fursa ya kutembelea Bunge la Uingereza, likijumuisha House of Commons na House of Lords, ambapo walijifunza kuhusu utendaji wa kila chombo cha kutunga sheria, utaratibu wa vikao, na historia ya Bunge hilo lenye asili ndefu katika demokrasia ya kisheria.

Uzoefu huo umefungua ukurasa mpya katika mpango wa OCPD wa kuboresha mifumo ya ndani, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria, Urekebu wa sheria,Ufasili wa sheria na usimamizi wa kumbukumbu.

Maafisa hao kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Tanzania wakipata wasilisilisho walipotembelea Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka ya Uingereza  (The National Archives) wakijifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker, unaotumika katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria nchini Uingereza.
Maafisa hao kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Tanzania wakipata wasilisilisho walipotembelea Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka ya Uingereza  (The National Archives) wakijifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker, unaotumika katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria nchini Uingereza.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad