-Waahidi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefikisha umeme katika vitongoji 2,354 kati ya vitongoji 3,421 Mkoani Mtwara huku ukiendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vilivyosalia mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa miradi ya REA Mkoani Mtwara, Mhandisi Daniel Mwandupe Oktoba 18, 2025 Wilayani Newala mkoani humo wakati wa kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kuunganishiwa umeme na kuutumia kujiletea maendeleo.
“Kwa Mkoa wa Mtwara hadi sasa tunaendelea kutekeleza miradi mikubwa miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 73.5 ya kusambaza umeme katika vitongoji 611 kati ya vitongoji 1,067 vilivyosalia,” alibainisha Mhandisi Mwandupe.
Akizungumzia mradi kusambaza umeme katika Wilaya hiyo ya Newala, Mhandisi Mwandupe alisema jumla ya vitongoji 39 vitafikishiwa umeme kupitia Mradi wa ujazilizi 2C kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 4.7.
“Leo tupo hapa Newala tunatekeleza mradi wa ujazilizi unaotekelezwa na Mkandarasi Mzawa Kampuni ya Sengerema ambaye pia anatekeleza mradi katika wilaya zingine Mkoani Mtwara kwa gharama ya shilingi bilioni 56 na anafikisha umeme katika vitongoji 461 ndani ya Wilaya za Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Tandahimba na Newala,” alisema Mha. Mwandupe.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Jaina Msuya alitoa wito kwa wananchi waliofikiwa na mradi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme ili kujiletea maenedeleo.
“Miradi ya umeme inakuja na fursa nyingi kuanzia hatua za awali za utekelezaji wa mradi hadi mradi unapokamilika kwani mkandarasi atapangoisha nyumba zetu, atafanya manunuzi mbalimbali, atatoa ajira; umeme unaweza kubadilisha maisha yenu, miradi ya umeme ni miradi ya kuwezesha wananchi kiuchumi,” alisisitiza Msuya.
Aliwasisitiza wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya umeme hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa miradi hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Kitongoji cha Amkeni Wilayani Newala, waliipongeza Serikali kwa kufikisha umeme na waliahidi kuwa walinzi wa miundombinu na wataendelea kuhamasishana kuunganisha umeme ili kubadilisha maisha yao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Amkeni, Sharifu Said alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza kwa kuwafikishia umeme wananchi wa kitongoji cha Amkeni.
Alisema kufika kwa umeme katika kitongoji hicho kutaleta maendeleo kwani wananchi wataanzisha viwanda vidogovidogo na fursa nyingine za kiuchumi zitaibuliwa na hivyo kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana katika kitongoji hicho.
Naye mkazi wa kitongoji cha Amkeni, Dativa Raimond ambaye ni mjasiriamali wa kuuza vinywaji alipongeza uwepo wa mradi huo ambao alisema umemuwezesha kuunganisha umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 pekee na alisema kuwa anatarajia kupitia umeme itamuwezesha kuongeza mauzo kwani ataanza kuuza vinywaji baridi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wake Awadh Ekoni Mkazi wa Kitongoji cha Amkeni mwenye umri wa miaka 70 alisema tangu amezaliwa hajawahi kuona umeme na aliipongeza Serikali kwa kufikisha mradi katika kitongoji hicho.







No comments:
Post a Comment