HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 27, 2025

Ulega Afunga Kampeni Mkuranga, Awaomba Wananchi Wamchague Dkt. Samia na Wagombea Wote wa CCM


Mkuranga, 26 Oktoba 2025 —
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdallah Ulega, leo amefunga rasmi kampeni zake za ubunge na kuwaomba wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Godauni, Kata ya Mkuranga, Mheshimiwa Ulega aliwataka wananchi waendelee kuiamini kazi kubwa inayotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Mkuranga haijawahi kushuhudia kasi ya maendeleo kama ilivyo sasa.

“Asiyeshukuru kwa yai, hata jogoo hachinjiwi. Nendeni mkamchague Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkanichague mimi kijana wenu, pamoja na madiwani wetu wa kata zote za Jimbo la Mkuranga,” alisema Ulega.

Ulega alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Wilaya ya Mkuranga imepata miradi mikubwa ya maendeleo kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji na barabara.

Aidha, Mgombea huyo wa CCM alitumia mkutano huo kuwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha uchaguzi mkuu utafanyika kwa amani, utulivu na haki, bila mwananchi yeyote kudhurika.

“Serikali haiwezi kuruhusu haki ya wananchi kupiga kura ivurugwe na watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza taharuki. Tumewekeza kwa kiwango kikubwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia unaimarishwa,” aliongeza Ulega.

Ulega alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Mkuranga kudumisha amani na umoja wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, akisisitiza kuwa maendeleo yaliyofikiwa ni matokeo ya uongozi bora wa CCM na ushirikiano wa wananchi.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad