TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imewataka wazazi na walezi kutowanyima watoto wao fursa ya kupata elimu nje ya mfumo ramsi bidi wanapofeli mitihani yao au kupata ufaulu mdogo huku ikisisitiza kuwa hiyo ndio njia mbadala kwa kundi hilo kutimiza malengo yao.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Meneja wa TEWW kampasi ya Dar es Salaam, Dk. Joshua Mushi wakati wa mahafali ya 19 ya wanafunzi wa kidato cha nne Shule Huria ya Ukonga Skillfull.
Dk. Mushi amesema mwanafunzi akianguka au kupata ufaulu mdogo si mwisho wa safari yake ya kielimu kwani anaweza kufikia malengo aliyojiwekea kwa kusoma nje ya mfumo rasmi na akapata ujuzi utaoamuwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Anayepata ufaulu mdogo au anayefeli kabisa atambue kuwa huo si mwisho wa safari yake ya kielimu, ipo fursa nje ya mfumo rasmi wa elimu, Shule Huria kama Ukonga Skillfull ni mfano mzuri sana ambao mwanafunzi anaweza kupata elimu hapo na kuendeleza malengo yake aliyojiwekea.
“Mwanafunzi anayesoma Ukonga Skillfull na anayesoma kwenye mfumo rasmi wote wanaweza kukutana vyuo vikuu ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) au chuo kikuu chochote duniani kwa sababu wote hao watakuwa na sifa zinazofanana,” amesema Dk. Mushi
Hata hivyo Dk. Mushi amewataka wadau wengine wanaotoa elimu nje ya mfumo rasmi kuhakikisha wanafuata taratibu ikiwemo kuvisajili vituo vyao.
Amesema Shule Huria ya Ukonga Skillfull imesajiliwa na inafanya kazi ya kutoa elimu kwa mujibu taratibu na sheria zilizopo nchini na kwamba utoaji wa elimu wa shule hiyo unatambulika na serikali.
“Niwapongeza Ukonga Skillfull kwani ni moja ya shule chache huria nchini ambayo inafanya vizuri, ina miongozo, waajiriwa zaidi ya 70 na matawi matatu ambayo yote yanafanyakazi, wadau wengine wanaotoa elimu nje ya mfumo rasmi waje kujifunza katika shule hii,” amesema
Aidha amesisitiza TEWW imekuwa ikiratibu utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi ambao unafanywa na wadau mbalimbali kwa kuwaongoza na kuwapatia miongozo kama ambavyo sheria inawataka.
“Pia tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali kwa kuangalia utolewaji wa elimu hiyo ya nje ya mfumo rasmi, changamoto zinazowakabili wadau wanaotoa elimu hiyo pamoja na kutoa mapendekezo ya maboresho,” amesema
Naye Muasisi na Mwanzilishi wa Shule hiyo ya Huria Ukonga Skillfull, Diodorus Tabaro amesema jumla ya wanafunzi 206 kutoka shule hiyo yenye matawi matatu sasa wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Amesema kwa mara ya kwanza wamefanya mahafali hayo kwa wanafunzi wa kidato cha nne na wanaorudia mitihani ya kidato cha nne kutoka katika matawi yao matatu ambayo ni Ukonga Skillfull makao makuu Gongo la Mboto, Mbezi Luis na Tegeta.
"Wahitimu hawa tumewaandaa vizuri na wapo tayari kwa ajili ya mtihani wa taifa, tunazidi kuwaombea na kwa sababu tumekuwa na rekodi nzuri ya matokeo, tunaimani kuwa watoto wetu watakwenda kufanya vizuri, tunazidi kuwakaribisha wanaotaka kurudia mitihani yao au kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kuja shueni kwetu.
“Sisi falsafa yetu ni kutoa elimu yenye kuleta mabadiliko chanya ya kitabia na tunaamini ili mwanafunzi aweze kufanikiwa vizuri lazima tabia yake ikae vizuri na ndio maana tuna vipindi vingi vya ushauri na wanabadilika, matokeo ya taifa ya wahitimu hawa yanakwenda kuwa mazuri,” amesema Tabaro
No comments:
Post a Comment