Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), jana tarehe 03 Oktoba, 2025 imeteketeza jumla ya kilogramu 4,402.02 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam.
Kati ya dawa za kulevya zilizoteketezwa ni kilogramu 2,168.18 za methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilogramu 515.48 za bangi na kilogramu 653.74 za mirungi. Dawa hizo zilizoteketezwa zilikuwa zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali ya kesi zinazohusu dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya uteketezaji kuanza, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, inayotaka vielelezo vya aina hiyo kuharibiwa wakati kesi ikiendelea au baada ya hukumu kutolewa.
“Mahakama iliagiza dawa hizo ziteketezwe kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo, kama Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 inavyotaka vielelezo vya dawa za kulevya kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa,” ilieleza Kamishna Jenerali Lyimo.
Miongoni mwa dawa za kulevya zilizoteketezwa huku mashauri yakiendelea makahamani ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed, iliyohusisha dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 882.71 na dawa ya kulevya aina ya methamphetamine kiasi cha kilogramu 2,167.29.
Aidha, dawa za kulevya zilizoteketezwa wakati mashauri yanayohusina na dawa hizo yalishatolewa hukumu na washitakiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo ni pamoja na kesi ya Hassan Azizi, Salum Shaaban Mpangula na Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo”, waliohukumiwa kifungo cha maisha jela, huku Gumbo Ramadhani Ally akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka kifungo cha miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy kifungo cha miaka mitatu jela.
Vilevile Kamishna Jenerali Lyimo aliwaonya wanaofanya biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani Mamlaka haitawafumbia macho.
“Mamlaka itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji ili kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya” alisema Lyimo.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupiga vita dawa za kulevya huku ikisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja.
Saturday, October 4, 2025

Home
Unlabelled
Tani 4.4 za dawa za kulevya zateketezwa Dar
Tani 4.4 za dawa za kulevya zateketezwa Dar
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment