Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni miongoni mwa masuala muhimu ya kuzingatia ili kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi.
PURA imesema hayo Oktoba 15, 2025 katika Kijiji cha Ruvula Mkoani Mtwara, wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya mradi wa uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotarajiwa kutekelezwa katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mkoani humo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mjiolojia Mwandamizi kutoka PURA Bw. Ebeneza Mollel amesema kuwa, pamoja na kudhibiti shughuli za kitalaamu, PURA pia inahakikisha wananchi wanajengewa uelewa wa miradi kabla ya kuanza utekelezaji.
“Sisi kama Mamlaka tunahakikisha kuwa, jamii zinazoishi au zinazozunguka maeneo ambayo miradi ya mkondo wa juu wa petroli inatekelezwa, zinashirikishwa kikamilifu katika miradi hiyo na kujengewa uelewa wa kina kuhusiana na mradi” alisema Mollel.
Sambamba na hilo, Bw. Mollel alisema kuwa, PURA inafuatilia kwa karibu hatua zote za utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia na kuwakumbusha watekelezaji wa mradi umuhimu wa utoaji wa uelewa wa mradi kwa wananchi.
Zoezi la utoaji wa uelewa wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay linafanywa katika vijiji vitatu ambavyo ni Ruvula, Msimbati na Mtandi vilivyopo katika Kata ya Msimbati, Mtwara.
Mradi huo unaohusisha uchimbaji wa visima viwili vya uzalishaji na kisima kimoja cha utafiti unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 80.2 unatekelezwa na Kampuni ya Maurel et Prom Tanzania kwa kushirikiana na TPDC.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba 2025 ambapo utawezesha, pamoja na mambo mengine, ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 30 kwa siku.
Ongezeko hilo litasaidia upatikanaji wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, kwenye viwanda, majumbani na kwenye vyombo vya usafiri (magari na bajaji).
No comments:
Post a Comment