NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewezesha ununuzi wa vifaa na mavazi ya michezo kwa timu ya NEMC ikiwa ni maandalizi ya kushiriki katika mashindano ya SHIMMUTA ya Mwaka huu yatakayofanyika kuanzia Tarehe 13 hadi 28 Novemba 2025.
Mavazi hayo yamebeba nembo ya NEMC na Adaptation Fund pamoja na jumbe fupi za kuhamasisha jamii kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 28, 2025 Jijini Dar es Salaam, Dkt. Immaculate Semesi amesema ubunifu huu unafanya michezo kuwa jukwaa la elimu na hamasa, kwa kuunganisha afya, ushirikiano na uelewa wa mazingira ili kuwasilisha ujumbe wa Tanzania kuhusu kujenga ustahimilivu wa taifa dhidi ya athari za tabianchi.
"Hizi juhudi zitakazokwenda sanjari na mkutano wa Umoja wa mataifa wa Mabadiko ya Tabianchi utakaofanyika Belem, Brazil kuanzia Tarehe 3-21 Novemba 2025, ambapo pia Mkurugenzi Mkuu wa NEMC nitashiriki kama mwakilishi katika ujumbe wa Serikali.
Aidha amesema kuwa ushiriki wa NEMC katika michezo ya SHIMMUTA ni fursa muhimu ya kuifikia jamii pana zaidi ikiwemo watumishi wa Umma, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
"Kupitia jukwaa hili, NEMC inaonesha namna uelewa na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kuunganishwa katika nyanja zote za maisha ya kijamii na kikazi, hivyo kuimarisha ushiriki wa wadau na kuibua taswira chanya ya Taasisi". Amesema
Amesema NEMC inafanya program za kuelimisha jamii na kutoa taarifa za maendeleo ya shughuli zake zikiwemo za utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Adaptation Fund.
Kwa upande Mkurugenzi wa fedha na utawala NEMC Bw.Dickson Mjinja amebainisha kuwa awamu hii wamejipanga kushindana na si tu kushiriki katika mashindano hayo ya wafanyakazi kwani tayari wameshafanya michezo ya kirafiki na taasisi kadhaa.
"Maandalizi ambayo tumefanya tumekuwa tukishirikiana na taasisi mbalimbali washindani wetu tumefanya mashindano ya majaribio na taasisi kama TBS nao pia tumeona uwezo wao lakini kwa uwezo wetu mkubwa tumekuwa tukishindana ipasavyo"amesema.
Mbali na hayo ameeleza kuwa ushiriki wao katika michezo hiyo itakuwa ni fursa ya kuwafikia wadau wao kwenye mashindano hayo ya wafanyakazi SHIMMUTA kupitia ufadhili wa mradi wa Adaptation Fund ili kujenga uhusiano mzuri wa kitaasisi baina yao.
Naye ,Mwenyekiti wa michezo NEMC BW. Fortunatus Patrick Amewashukuru wafadhili wao ambao ni mfuko wa ufadhili wa mabadiliko ya tabia ya nchi (Adoptation Fund)kwa kuwapatia vifaa hivyo vya michezo kwani ni moja ya mikakati ya taasisi hiyo kuhusiana na jamii zikiwemo taasisi nyingine kwa njia nyingi ikijumuisha michezo kwa lengo la kuhakikisha majukumu yake yanafahamika.























No comments:
Post a Comment