HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 11, 2025

Ndemanga Awataka Wananchi Chalinze Kuacha Kuuza Ardhi kwa Bei Duni

 

Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akikabidhi Hati kwa Mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata huduma katika Kliniki Hiyo.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Bw. Rugambwa (kulia), akimpa maelezo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga, wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi katika Halmashauri ya Chalinze, mkoa wa Pwani, Oktoba 11, 2025.
Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri, Bw. Egidius S. Kashaga, akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga, alipokuwa akitembelea maeneo ya utoaji huduma kabla ya uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi.
Baadhi ya wananchi wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa wa Kliniki ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze tarehe 11/10/2025 iliyoandaliwa kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja Mkoani Pwani.

Na Lusajo Mwakabuku – WANMM, Chalinze

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga, amewaasa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuacha kuuza maeneo yao kwa bei isiyoendana na thamani ya soko, akibainisha kuwa ardhi ya mkoa wa Pwani kwa sasa ni rasilimali muhimu kutokana na ongezeko la uwekezaji.

Akizindua rasmi Kliniki ya Ardhi inayofanyika Halmashauri ya Chalinze leo (11 Oktoba 2025), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Ndemanga amesema wananchi wanapaswa kutambua thamani ya maeneo yao na kutumia fursa ya kupata elimu kupitia kliniki hiyo.

“Naomba kuwaambia wazee wangu mliopo hapa na wengine muwapelekee habari hii, acheni kuuza maeneo yenu kiholela. Soko la ardhi mkoani Pwani linaendelea kukua kwa kasi, kumbukeni Dar es Salaam imeshajaa na sasa inapumulia huku kwetu. Ardhi ni mtaji wa uwekezaji na utajiri iwapo mtaitumia ipasavyo,” alisema Ndemanga.

Aidha, alisisitiza kuwa wananchi wasioweza kuyaendeleza maeneo yao, wanapaswa kufika ofisi za ardhi au kliniki hiyo ili wapatiwe ushauri juu ya thamani halisi ya ardhi, badala ya kuuza kwa bei ya hasara.

“Kuna mzee mmoja hapa jirani nimeshuhudia watoto wake wakilalamika kuwa kauza eneo kwa shilingi laki moja na nusu. Hii ni fedha ndogo sana ikilinganishwa na thamani ya eneo husika, hasa wakati huu ambapo fursa za uwekezaji zimefunguka,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Chalinze, Bw. Deo Msilu, akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, alisema Kliniki ya Ardhi ilianza Oktoba 7 na itafanyika kwa muda wa wiki mbili kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani.

Msilu alibainisha kuwa kliniki hiyo ni mwendelezo wa zoezi la uboreshaji wa usalama wa milki za ardhi lililoanza Juni 2024, ambapo hadi Machi 30, 2025 kata tatu za Bwilingu, Pera na Vigwaza zilikuwa zimetambua jumla ya vipande vya ardhi 24,730, huku viwanja 23,936 vikiwa vimepimwa.

“Wananchi zaidi ya 500 wameshahudumiwa kupitia kliniki hii, wakipata huduma za elimu ya ardhi, utatuzi wa migogoro, upimaji, umilikishaji na ugawaji wa hati miliki kupitia mfumo wa kisasa wa eArdhi ambao umeharakisha sana huduma,” alisema Msilu.

Kwa mujibu wa viongozi hao, kliniki hizo zimepunguza changamoto za muda mrefu za wananchi kuhusu umilikishaji ardhi na zinatarajiwa kuongeza thamani ya maeneo ya Chalinze, sambamba na kuvutia wawekezaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad