Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amezindua toleo la 24 la Mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro Premium Lager.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, uliofanyika Oktoba 17, 2925 Mpogolo amesema mbio hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza utalii wa michezo, jambo ambalo limekuwa mada muhimu duniani kwa sasa.
Aidha ametoa changamoto kwa waandaaji wengine wa matukio ya michezo kuiga mfano wa Kilimanjaro Premium Lager Marathon, ambayo imeendelea kudumu kwa miaka 24 huku ikishirikiana vyema na Serikali.
“Nimeambiwa kuwa kupitia mbio hizi, wanariadha mahiri kama Alphonce Simbu, mshindi wa Mashindano ya Riadha Duniani yaliyofanyika Tokyo mwaka huu, alipata uzoefu na kutambulika kimataifa kutokana na kipaji chake cha kipekee kupitia ninyi” amesema Mpogolo
Ameongeza kuwa mafanikio ya wanariadha kama Simbu yanapaswa kuwa hamasa kwa wengine kushiriki katika mbio hizo ili kukuza vipaji vya ndani na kutoa mabingwa zaidi kwa Tanzania.
Mpogolo amesema mbio za marathoni zimekuwa tukio kubwa la kimichezo nchini na jukwaa muhimu la kutangaza utalii.
“Tunajivunia mbio hizi kwa kuwa zinawakutanisha washiriki zaidi ya 13,200 na watazamaji kutoka zaidi ya nchi 60, wote wakiwa watalii. Hii ni hatua kubwa kwa taifa,” amesisitiza.
Aidha, amebainisha kuwa tukio hilo limekuwa chachu ya ustawi wa biashara katika kipindi cha mashindano kutokana na wingi wa wageni wanaotembelea Moshi na maeneo jirani.
“Nawapongeza wadhamini wote wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu wa Mbio za Km 42), YAS (Km 21), na CRDB Bank (Mbio za Burudani za Km 5). Pia nawashukuru wadhamini rasmi Kilimanjaro Water na TPC Sugar; wabia rasmi —GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement na ALAF Limited; pamoja na wasambazaji rasmi Salinero Hotel, Kibo Palace Hotel Arusha, na Keys Hotel Moshi. Bila nyinyi, haya yote yasingewezekana,” amesema.
Ametoa pia wito kwa washiriki na watazamaji kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii kama Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, na Zanzibar, vinavyoendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Khensani Mkhombo amesema wanajivunia kudhamini mbio hizo kwa miaka 24 mfululizo kupitia Kilimanjaro Premium Lager, jambo linaloonyesha dhamira ya kampuni hiyo katika kukuza utalii na utamaduni wa Watanzania.
Ametoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema kupitia tovuti rasmi www.kilimanjaromarathon.com au Mixx by YAS, kwani usajili utaanza Jumatatu, Oktoba 20.
Mkhombo ameongeza kuwa washiriki watarajie wikendi ya furaha, na akawahimiza wageni na wakazi wa Kilimanjaro kupanga kukaa Moshi kwa muda mrefu ili kufurahia matukio ya Kilimanjaro Premium Lager.
Naye Meneja Mawasiliano wa YAS, Christina Murimi, amesema “YAS inajivunia kurejea kama mdhamini rasmi wa mbio za kilomita 21 kwa mwaka wa 11 sasa. Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya kuunganisha na kuwezesha jamii kote Tanzania kupitia teknolojia zetu za 4G na 5G.”
Ameongeza: “Nawaalika wote kuungana nasi kukimbia, kusherehekea na kuenzi ari ya Tanzania kwenye mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro 2026.”
Waandaaji wa tukio hilo waliwataka washiriki kununua tiketi mapema ili kuepuka usumbufu dakika za mwisho na kujiandaa vyema kwa tukio litakalofanyika Jumapili, Machi 22, 2026, katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).
Mbio hizo zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited, huku kampuni ya Wild Frontiers Events ikisimamia matangazo na shughuli za usafiri wa ndani wa tukio hilo.


Meneja Mawasiliano wa YAS, Christina Murimi akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2026 Jijini Dar es Salaam

Meneja wa CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Muhumuliza Buberwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kilimanjaro Marathon jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Khensani Mkhombo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2026 Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment