
Na Mwandishi Wetu, West Kilimanjaro
Jamii imetakiwa kushirikiana kikamilifu katika kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda urithi wa asili wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji wa mazingira “Go Green, Save Nature” uliofanyika katika Shamba la Miti West Kilimanjaro hivi karibuni.
“Changamoto nyingi zinazotukabili leo zinatokana na uharibifu wa mazingira. Ni jukumu letu sote kupambana kulinda uoto wa asili ili kuendelea kunufaika na rasilimali zetu,” alisema Dkt. Timbuka.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mfuko wa Ruzuku Ndogo wa Mazingira Duniani (GEF/SGP/UNDP), Faustine Minga, alitoa rai kwa jamii kushirikiana kuhakikisha dunia inabaki salama kupitia jitihada endelevu za utunzaji wa mazingira.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, PCO Robert Faida, alisisitiza ushirikiano kati ya jamii na taasisi za uhifadhi akisema:
“Tunashirikiana na jamii kupitia kampeni hii ya Go Green ili kuhakikisha uoto wa asili unarejea na kuendelea kudumu kwa vizazi vijavyo.”
Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Mrisho Mabanzo, alisema elimu kwa lugha rahisi inatolewa ili kila mmoja aelewe umuhimu wa kushiriki katika jitihada za kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni hiyo na Afisa Utalii wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, Mensier Elly, aliwashukuru wadau kwa kushirikiana na kusisitiza kwamba kampeni inalenga kupanda miti ya asili kwenye maeneo yaliyoungua, kupanda miti ya matunda katika shule zinazozunguka Mlima Kilimanjaro ili kuboresha lishe za wanafunzi, kufanya usafi wa njia za watalii na kambi za wageni, pamoja na kufungua fursa za MICE Tourism (Utalii wa Mikutano).
Aidha, Mratibu wa Connecting Youth Connecting Africa – Kenya, Ruth Omobe, pamoja na kamati ya maandalizi walimshukuru Mratibu wa Taifa wa GEF/SGP/UNDP Tanzania pamoja na wadau mbalimbali akiwemo Zara Tanzania, Bonite Bottlers, Notice Kilimanjaro, Altezza Travel, Aviagen East Tanzania, Trek & Hide Adventures na wengine kwa mchango wao muhimu katika kufanikisha tukio hilo.
Kwa niaba ya Connecting Youth, Connecting Africa na kamati ya maandalizi ya kampeni hiyo, waandaaji walisema kuwa kampeni imekuwa chachu kubwa ya kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa misitu na kuongeza nguvu za vijana katika kulinda urithi wa asili wa nchi.
Kauli mbiu ya kampeni hiyo imesisitiza mshikamo wa jamii:
“Pamoja tunaweza kujenga kizazi kinachothamini mazingira na kuchukua hatua endelevu — Go Green, Save Nature.”
MATUKIO YA UPANDAJI WA MITI NA UGAWAJI WA VYETI VYA SHUKRANI.

Mbali na wageni pamoja na wanafunzi kupatiwa vyeti kulikuwa na zoezi la kufanya usafi katika Mt.Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment