Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amewataka wananchi wa Jimbo la Busanda mkoani Geita kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika eneo hilo.
Biteko alitoa wito huo wakati akihitimisha kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda, Dk. Jafari Rajabu Seif, katika viwanja vya Wachina, Kijiji cha Bugogo, Kata ya Bukoli, Wilaya ya Geita.Amesema anamfahamu Dk. Jafari kama Kiongozi makini, mchapakazi na mwenye moyo wa kujituma katika kutatua changamoto za wananchi.
“Namfahamu vizuri mgombea wenu kabla hata hajawa mgombea. Kiukweli, Busanda mmempata mtu sahihi kabisa kwa maendeleo ya jimbo lenu,” alisema Biteko.
Aidha, Biteko aliwaomba wananchi kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, akisema serikali yake imeonesha dira ya kweli ya maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Busanda, Dk. Jafari Rajabu Seif, aliwaeleza wananchi namna ilani ya chama hicho inavyotekelezwa kwa vitendo ndani ya jimbo hilo.
Alitaja baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya lami ya Geita–Kakola na mradi mkubwa wa maji utakaoondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika kata mbalimbali za Jimbo la Busanda.
“Serikali ya CCM imejipanga kuhakikisha changamoto zote muhimu zikiwemo za barabara, afya na maji zinatatuliwa ndani ya muda mfupi. Nawaomba mnipatie ridhaa niendelee kuwatumikia kwa ufanisi zaidi,” alisema Dk. Jafari.







No comments:
Post a Comment