HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 28, 2025

BIL 860 ZINATUMIKA UJENZI MIRADI YA DHARURA NCHINI -ENG MOHAMED BESTA

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea na ujenzi wa mpango wa dharura uliaoanzishwa chini ya TANROADS kufuatia maafa ya mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi Mei 2024.

Mradi unatekelezwa chini ya miradi mikubwa inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo TanTIP, RISE, MBDP na dirisha la CRW huku lengo kuu la mradi ikiwa ni kurejesha mawasiliano ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa, ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu na shughuli za kiuchumi ziendelee bila usumbufu.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huu, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa Ujenzi wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya dharura inayotekelezwa katika mikoa 22 ya Tanzania Bara ikihusisha miradi 81 ya dharura ambayo inahusisha ujenzi na ukarabati wa madaraja, barabara, mitaro na makaravati yaliyoharibiwa.

Amesema kuwa jumla ya fedha zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ni Dola za Marekani milioni 325 (sawa na takribani Shilingi bilioni 840) ambazo zinatekeleza miradi hiyo chini ya mpango wa CERC (Contingency Emergency Response Component), ambapo inatekelezwa na makampuni ya wakandarasi wazawa 70 na makampuni 11 kutoka nje ya nchi.

Mhandisi Besta amesema kwa sasa, maendeleo ya utekelezaji yapo katika wastani wa asilimia 68 ambapo miradi 12 imekamilika kwa zaidi ya asilimia 95 hadi 100, na miradi mingine 53 ipo kati ya asilimia 50–95 ya utekelezaji.

Ameyataja mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa kuwa ni pamoja na kurejeshwa kwa mawasiliano katika maeneo mengi yaliyokuwa yamekatika kutokana na mafuriko, Kuimarika kwa miundombinu ya barabara na madaraja katika mikoa 22, hivyo kuongeza usalama na kuharakisha huduma za kijamii na kiuchumi, Kujenga uwezo wa wakandarasi wazawa kupitia ushiriki wao kwenye kazi za dharura na Kuimarisha uratibu kati ya TANROADS, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia katika kushughulikia majanga kwa haraka zaidi.

Amesema kuwa TANROADS imeweka mikakati ya kudumu katika kukabiliana na majanga ya miundombinu (kama mafuriko au maporomoko) ambapo imeanza Kuimarisha usanifu wa miundombinu kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, Kuanzisha mpango wa tahadhari na maandalizi mapema (early warning systems) ili kujibu haraka wakati wa maafa, Kuhakikisha miradi mipya inazingatia viwango vya juu vya uthabiti (resilience) dhidi ya mafuriko na Kujenga uwezo wa wataalam wa ndani na kuendelea na ushirikiano na Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad