HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 18, 2025

ZEC YATANGAZA KURA YA MAPEMA KUPIGWA OKTOBA 28

 





Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar.

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza rasmi ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambao utahusisha uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George J. Kazi, amesema kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 34(3) na (4) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018, Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo, kutakuwepo na upigaji kura za mapema ambao utafanyika Jumanne, Oktoba 28, 2025, ikiwa ni siku moja kabla ya upigaji kura mkuu. Upigaji kura huo maalum utawawezesha watendaji na Askari wanaosimamia shughuli za uchaguzi kupiga kura kabla ya siku ya wananchi wote kupiga kura.

Kura za mapema zitawahusisha Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Vituo, Wasaidizi wa Uchaguzi, Askari Polisi walioko kazini, pamoja na Wajumbe na Watendaji wa Tume ya Uchaguzi.

Kazi amesema “Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa watumishi wanaosimamia zoezi la uchaguzi hawakosi nafasi ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura”

Kwa mujibu wa ZEC, maandalizi ya uchaguzi yameanza mapema ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi, amani na usalama. Tume imesisitiza kuwa inaendelea kushirikiana na vyama vya siasa, asasi za kiraia pamoja na wadau wa kimataifa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki.

Vilevile, wananchi wametakiwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano wakati wa kuelekea uchaguzi huo. Tume imetoa wito kwa wapiga kura wote kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 ili kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad