Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameipongeza Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano uliofanikisha Serikali ya Awamu ya Sita kupata mafanikio katika sekta za Kazi, Vijana, Ajira, Watu wenye Ulemavu na kinga ya Jamii.
Ameeleza mafanikio hayo wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo leo Agosti 21, 2025 ikiwa na lengo la kuwashukuru watumishi na kuwapongeza kwa kutekeleza shughuli kwa ufanisi na tija katika kipindi chote alicho hudumu na kuiongoza Ofisi.
Mheshimiwa Ridhiwani amesema kuwa katika miaka minne ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisi imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 18 hadi 9, kutoa vibali 55,642 kwa wageni waliokuja kufanya kazi na kupunguza muda wa utoaji wa vibali vya kazi kutoka miezi miwili hadi siku 14.
Mafanikio mengine, Ofisi imefanikiwa kutoa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana yenye thamani ya shilingi bilioni 3.2 kwa zaidi ya vijana 164,000, Serikali imezalisha ajira zaidi ya milioni 8 kupitia miradi ya Bomba la Mafuta, Reli ya Kisasa (SGR) na bwawa la Nyerere. Vilevile, Serikali imefanikiwa kupandisha pensheni ya chini kutoka shilingi 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi.
Mheshimiwa Ridhiwani ameeleza mafanikio mengine kuwa ni kuwapeleka watanzania 7,907 kwenye ajira nje ya nchi na kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 121,526 katika sekta za kilimo, TEHAMA na ujenzi, na mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa vijana 22,176 kupitia utarajali.
“Mafanikio yaliyopatikana si ya Taasisi peke yake bali ni ya kila mtumishi aliyehusika kwa namna moja au nyingine” alisisitiza Waziri Kikwete na kuongeza kuwa watumishi waongeze ubunifu, matumizi ya TEHAMA, uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga akizungumza kwenye kikao hicho amesema Ofisi hiyo imefanikiwa kuandaa nyaraka mahsusi za utendaji kazi ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya (2007), Toleo la mwaka 2024; Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na mkakati wake;; Mpango kazi wa Taifa Haki na Ustawi kwa Watu Wenye Ualbino 2024/2025 – 2028/2029 (MTHUWWU);Mpango maalum wa Vifaa Saidizi (NATS)
Ameongeza kuwa, Miongozo na mifumo mingine ni Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu; Mwongozo wa Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri, Mwongozo wa Wakala Binafsi wa Ajira; Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za soko la Ajira, Mfumo wa uratibu wa Kinga ya Jamii 2025 na Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Taarifa za Soko la Ajira.
No comments:
Post a Comment