HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 8, 2025

Wafungwa 170 wahitimu mafunzo ya ujasiriamali kupitia IAA

 





Mwandishi Wetu,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Innocent Bashungwa amewatunuku vyeti vya kuhitimu wafungwa 170 waliokuwa wakipata mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Ameyasema hayo katika hafla ya kutunuku vyeti vya ujasiriamali na stadi za biashara kwa wafungwa waliohitimu mafunzo hayo huku akimpongeza Mkuu wa Chuo -IAA Profesa Eliamani Sedoyeka, pamoja na menejimenti ya chuo kwa umahiri na ubinifu kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara kwa wafungwa.

Kadhalika amekitaka IAA kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza kutekeleza mara moja mpango wa kuanzisha kituo cha umahiri cha utoaji wa mafunzo kwa wafungwa ili kuwapa maarifa, ujuzi na stadi za biashara zitakazowawezesha kujikimu kiuchumi pindi wanapomaliza vifungo vyao.

Mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara yalitolewa kuanzia Mei 7, 2025 kwa wafungwa takribani 170 wakiwemo wanawake 41 na wanaume 129.

“Kama Mkuu wa Chuo pamoja na timu yako naomba tuwapongeze na tuwashukuru kwa ushirikiano, ambao mnalipa Jeshi la Magereza Katika hii programu ambayo leo hii tunatunuku wahitimu 170” amesema

Aidha, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza CGP Jeremiah Katungu amesema ana imani kubwa kuwa wahitimu wa mafunzo hayo wamepata elimu na maarifa muhimu, yatakayowawezesha kuwa wabunifu na wajasiriamali mahiri pindi watakapomaliza vifungo vyao na kwenda kwenye jamii.

“Lengo la mafunzo ni kuwaandaa na kuwarejesha kwenye jamii wakiwa raia wema na wenye uwezo wa kuendesha shughuli za kiuchumi” amesema

Mkuu wa IAA, Profesa Sedoyeka amemshukuru CGP Katungu kwa mashirikiano mazuri na IAA katika urekebishaji wafungwa, kupitia utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara na kutoa rai kwa taasisi zingine za elimu, mashirika ya kiraia na taasisi binafsi kushirikiana na IAA katika kuhakikisha wafungwa wanapata ujuzi na maarifa.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo yaliyoanza Mei 7, 2025 wamepongeza viongozi wote na walimu kutoka IAA kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali na stadi za biashara, wakisema italeta tija kwao kiuchumi baada ya kumaliza vifungo vyao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad