KAIMU Meneja wa ya Forodha Mkoa wa Mara, Abdallah Mambi, ametoa wito kwa wananchi hasa wanaojihusisha na biashara za mipakani kuachana na magendo kupitia njia za panya na badala yake wapite katika miapaka rasmi, ili kufanya biashara halali na kuiwezesha serikali kukusanya kodi kwaajili ya maendeleo.
Meneja Mambi, alitoa wito huo, wakati wa ufunguzi wa semina ya mabadiliko ya Kibajeti yanayotokana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 kwa Maafisa Forodha, Mawakala wa Forodha ilifanyika Agosti 19, katika kituo cha Mpaka wa Sirari. "serikali itaendelea kutoa elimu kwa watumishi wa forodha, mawakala na wadau wa biashara kuhusu mabadiliko ya sheria ya fedha ili kuwezesha ulipaji bora wa kodi na kuondoa mianya ya magendo." Alieleza Mambi.
Akizungumzia umuhimu wa semina hiyo, Mambi alisema lengo la semina hizo ni kuhakikisha watumishi na wadau wanapata uelewa wa kina juu ya mabadiliko ya sheria za kodi zinazotolewa kila mwaka.
“Kupitia semina hii tumepata uelewa mkubwa wa mabadiliko yaliyofanywa na serikali..., Tunawahimiza wananchi na wafanyabiashara kuacha shughuli za magendo kwa sababu sheria zetu ni rafiki na zinarahisisha kufanya biashara kwa halali. Kodi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Mambi.
Kwa upande wake, Hasan Minga, Afisa Forodha Mkuu kutoka Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam na muwezeshaji wa semina hiyo, alisema serikali imekuwa ikipitia upya sheria za kodi kila mwaka ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuleta nafuu kwa wazalishaji wa bidhaa.
“Katika semina hizi tunawaeleza wadau nini kimebadilika, sera husika zina malengo gani na namna yanavyosaidia serikali kukusanya kodi kwa wakati. Lakini pia tunawaweka wazalishaji na mawakala wa forodha kwenye nafasi nzuri ya kutambua mabadiliko, ili waweze kuwashauri vizuri wateja wao na kutumia unafuu wa kikodi kuongeza uzalishaji,” alisema Minga.
Naye Robert Yusuf, wakala wa forodha kutoka kampuni ya … Logistics Ltd alisema kama kiungo muhimu kati ya TRA na wateja wao, mawakala wa forodha watahakikisha taarifa zote za mabadiliko ya kodi zinafika kwa wafanyabiashara ili kuwarahisishia shughuli za kuingiza na kutoa bidhaa katika mipaka ya forodha.
Aidha, Robin Sindani, wakala wa forodha Sirari, alisema mawakala wamepokea kwa furaha elimu hiyo na wataendelea kushirikiana na TRA katika kutoa mwongozo kwa wateja wao.
“Semina hii ni muhimu kwetu kwani inatusaidia kuwaelimisha wateja wetu kuhusu mabadiliko ya kodi, kulinda viwanda vya ndani na kuongeza export kuliko import. Tunaiomba TRA iwe inatufikia mara kwa mara kwa sababu wakati mwingine mabadiliko yanatokea kabla ya semina, hivyo tunakutana na changamoto ya kueleza wananchi mapema,” alisema Sindani.
Kwa pamoja, wadau hao walisema elimu hiyo inasaidia kuongeza uelewa wa mnyororo mzima wa kodi na kuwezesha wafanyabiashara kufanya biashara kwa uhalali, kukuza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.






No comments:
Post a Comment