HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 6, 2025

Tanzania Yatoa Wito kwa Washirika Kutimiza Ahadi zao kwa Maendeleo ya Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari

Tanzania imethibitisha uungaji mkono wake kwa dhati katika utekelezaji wa Mpango wa Awaza wa Utekelezaji na kutoa wito kwa washirika wote kutimiza ahadi zao kufadhili maendeleo ya miundombinu, kujenga uwezo, na kushughulikia vikwazo visivyo vya kiforodha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kyaharara, amesema hayo tarehe 6 Agosti,2025 alipozungumza katika majadiliano ya “Kuchangamkia Uwezo wa Mabadiliko Kupitia Biashara, Urahisishaji wa Biashara na Ujumuishaji wa Kikanda kwa Nchi zisizo na mlangoi wa Bahari”, kwenye Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa nchi zisizo na Mlango wa bahari unaoendelea katika mji wa Awaza nchini Turkmenstan.

Amesema Tanzania imechukua hatua kadhaa muhimu kwa lengo la kupunguza muda na gharama za usafirishaji, kuongeza muunganiko wa kanda, na kuboresha ushindani wa kibiashara kwa nchi zenye bahari na zile zisizo na mlango wa bahari.

"Tanzania imeweka mfumo wa Tanzania kisasa wa dirisha moja, jukwaa la kidigitali la huduma moja linalorahisisha taratibu za forodha na kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa wadau wote,” alisisitiza Prof. Kyaharara.

Ameongeza kuwa Bandari ya Dar es Salaam imeboreshwa kwa kuwekwa vifaa vya kisasa vya kushushia mizigo, kuchukua nafasi ya krane zilizochakaa, hivyo kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuleta tija. "Uboreshaji huu umehusisha kuongeza kwa kina cha bandari ya Dar es Salam hadi kufikia mita 15.5, pamoja na kupanua njia ya kuingilia meli, ili kuruhusu meli kubwa zaidi kuingia nnchini. Hii imewezesha Tanzania kunufaika na maboresho hayo na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafirishaji,” alisisitiza.

Prof. Kyaharara pia ameeleza kuwa Tanzania imeanzisha Vituo vya Pamoja vya Ukaguzi (One-Stop Border Post) ikiwa ni sera chini ya mwongozo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imepunguza vituo vya ukaguzi kutoka zaidi ya kumi hadi vitatu kwa sasa na kuongeza kuwa inalenga kuvimaliza kabisa ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa haraka zaidi.

Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), ambayo ni ya umeme yenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa na kwamba itakapokamilika, itawezesha mizigo kufika nchi zisizo na mlango wa bahari kwa muda wa chini ya saa 24, hivyo kuboresha kwa kiwango kikubwa muunganisho wa kikanda na kukuza biashara ya mipakani.

"Miradi mingi kati ya hii inatekelezwa kwa ushirikiano wa pande mbili na nchi jirani zisizo na mlango wa bahari kama Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Uganda, ili kuhakikisha kunakuwepo na manufaa ya pamoja na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda," alisisitiza Prof. Kyaharara.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad