Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, huku wakilinda amani, mshikamano na maadili ya kitaifa.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Jaji Mwambegele alisema waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya Tume na wananchi, hivyo wanayo nafasi ya kipekee ya kusaidia katika kutoa elimu ya mpiga kura, kufikisha taarifa sahihi, na kuchangia mchakato wa uchaguzi kwa weledi.
“Tume inawatambua ninyi waandishi wa habari kama daraja la mawasiliano kati ya Tume na umma, lakini pia kama wadau muhimu wa uchaguzi. Mnachangia kwa kiasi kikubwa kuripoti habari za maandalizi, kampeni, upigaji kura na matokeo,” alisema Jaji Mwambegele.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, NEC imeshatangaza ratiba rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Utoaji wa fomu kwa wagombea wa ubunge na udiwani utaanza Agosti 9 hadi Agosti 27, huku wagombea wa urais na makamu wao wakitarajiwa kuchukua fomu kati ya Agosti 14 hadi 24. Uteuzi wa wagombea wote utafanyika Agosti 27.
Kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 27 kwa upande wa Tanzania Bara, na hadi Oktoba 28 kwa upande wa Zanzibar. Jaji Mwambegele aliwaasa wanahabari kutumia vyombo vyao kuhamasisha kampeni za kistaarabu zinazojenga hoja na siyo chuki au uchochezi.
“Katika kipindi hiki cha kampeni, mnapaswa kuhakikisha kuwa vyombo vyenu havitumiwi kuvuruga amani ya nchi. Toeni taarifa za haki, za kweli, na zenye kujenga jamii,” alisisitiza.
Ameeleza kuwa mwaka 2024, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria mbili muhimu: Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, pamoja na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Kupitia sheria hizo, Tume imetunga kanuni na miongozo ya kuendesha uchaguzi wa mwaka huu.
Aidha, Tume imetoa mwongozo wa elimu ya mpiga kura, mwongozo kwa vyombo vya habari, na nakala za sheria husika kwa wadau wote, ili kuwawezesha kufuata taratibu ipasavyo.
“Nawasihi msome na kuelewa nyaraka hizi ili mchango wenu katika uchaguzi huu uwe wa manufaa kwa taifa,” alisema Jaji Mwambegele.
Kwa lengo la kuongeza weledi katika kuripoti shughuli za uchaguzi, Tume imeandaa mafunzo maalum kwa wahariri na waandishi wa habari yatakayofanyika Agosti 4, 2025.
Katika hotuba hiyo, Jaji Mwambegele alieleza kuwa kwa sasa kuna majimbo ya uchaguzi 272—yakijumuisha 222 kutoka Tanzania Bara na 50 kutoka Zanzibar. Kati ya hayo, majimbo nane ni mapya, na kata nne mpya zimeongezwa na kufikisha idadi ya kata zinazoshiriki uchaguzi kuwa 3,960.
“Tunawashukuru kwa ushirikiano wenu wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura uliofanyika Julai 2024 hadi Julai 2025. Tumeinufaika sana kupitia vyombo vyenu vya habari,” aliongeza.
Kwa upande mwingine, Tume imetoa vibali kwa taasisi na asasi 164 kutoa elimu ya mpiga kura, na taasisi 88 (76 za ndani na 12 za kimataifa) kufanya uangalizi wa uchaguzi.
Akihitimisha hotuba yake, Jaji Mwambegele aliwahimiza waandishi wa habari kuendeleza ushirikiano na Tume, kwa lengo la kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika kwa uhuru, haki, uwazi na kuaminika.
“Kauli mbiu yetu ni: ‘Kura Yako Haki Yako – Piga Kura.’ Tume ina matumaini makubwa ya kufanikisha uchaguzi huu kwa kushirikiana nanyi katika kila hatua,” alimalizia.
Baadhi ya washiriki wakihojiwa na vyombo vya habari.
Picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment