HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 21, 2025

NBAA YAWANOA WATAHINIWA MITIHANI CPA


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao pamoja na mafunzo ya ana kwa ana kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi, ikilenga kuongeza ufanisi na maandalizi bora kwa watahiniwa wake.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo kwa niaba ya  Mkurugenzi Mtendaji, Peter Lyimo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo, , alisema kuwa warsha hiyo imelenga kuwanoa wanafunzi wa ngazi mbalimbali kupitia mbinu bora za kujibu mitihani, hasa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa kwa watahiniwa.

“Yapo masomo ambayo kiwango cha ufaulu kimekuwa kidogo. Hivyo tumewaleta walimu kutoka vyuo na Taasisi mbalimbali ili watoe uzoefu na mbinu sahihi kwa watahiniwa, ili waweze kujiandaa vizuri,” alisema Lyimo.

Aidha, Lyimo alifafanua kuwa mbali na wanafunzi waliounganishwa kupitia mtandao, pia kulikuwa na kundi la wanafunzi waliofika moja kwa moja katika ofisi za Bodi (NBAA) kupata mafunzo hayo ya kitaalamu ana kwa ana. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi na kuwawezesha wanafunzi kuuliza maswali kwa urahisi zaidi na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa walimu.

Aliwasisitiza wanafunzi kuepuka kujiandaa kwa mazoea au kiholela na badala yake kutenga muda wa kutosha kujifunza, akibainisha kuwa kuna tofauti kubwa kati ya mitihani ya vyuoni na mitihani ya Bodi.

“Tumewasisitiza sana namna ya kujiandaa. Waweke muda wa kutosha kwenye kujifunza kwani mitihani ya Bodi inahitaji umakini mkubwa na maandalizi ya kitaalamu zaidi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Lyimo, NBAA imejipanga kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinapanda katika mitihani yake mbalimbali, sambamba na kuongeza uelewa wa watahiniwa, ili baada ya kumaliza mitihani waweze kuwa wataalamu waliobobea kwenye uhasibu na ukaguzi.

Bodi hiyo imesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha kila mtahiniwa anapata maandalizi stahiki na changamoto zinazowakabili zinapatiwa suluhisho la kudumu.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo Peter Lyimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi
Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka akiwakaribisha wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani mbalimbali ya Bodi ambao walikuwa wakisikiliza Warsha hiyo ana kwa ana na kwa njia ya mtandao.
Mkufunzi CPA Rashid Mganwa akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B2 na C1 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia ana kwa ana na kwa njia ya mtandao.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, CPA Dkt. Emmanuel Christopher akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B1 na C3 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia ana kwa ana na kwa njia ya mtandao.


Baadhi ya  wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi wakifuatilia mada pamoja na kuuliza maswai kwa wakufunzi.
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad