HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 14, 2025

Naibu Waziri Chumi Akoshwa na kiwango cha Ubunifu NM-AIST



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, ameonesha kuridhishwa kwake na kiwango cha ufanisi na ubunifu unaofanywa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya chuoni hapo jijini Arusha.

Katika ziara hiyo Mhe. Chumi alipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya taasisi hiyo na kujionea teknolojia mbalimbali zilizobuniwa kwa lengo kuongeza tija na ufanisi katika shughuli mbalimbali za uchumi na kijamii za wananchi, ikiwemo teknolojia ya kuchakata taka kuwa mbolea na nishati safi, uji lishe, chanjo ya samaki, teknolojia ya kukausha zao la tumbaku kwa nguvu ya mionzi ya jua na kemikali ya asili ya kuhifadhi ubora wa ngozi za wanyama.

Akizungumza na uongozi wa NM-AIST inayojihusisha na tafiti za kisayansi, uhandisi, teknolojia na ubunifu, Mhe. Chumi aliipongeza taasisi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini huku akisisitiza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na NM-AIST kupitia diplomasia ya uchumi ili kuhakikisha bunifu zinazozalishwa zinanufaisha Watanzania na kufahamika kimataifa.

Aidha Naibu Waziri Chumi ametoa wito kwa Mamlaka mbalimbali za Serikali nchini kuchangamkia bunifu za NM–AIST ili kuongeza ufanisi na tija kwenye shughuli za kila siku za kiuchumi za wananchini.

“Tunahamasisha halmashauri kote nchini kutumia teknolojia hizi, na kuangalia uwezekano wa kutumia bajeti zao kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye uhitaji maalum kuanzisha miradi ya kisasa kupitia bunifu hizi,” alisema Mhe. Chumi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, alisema taasisi hiyo imekuwa ikiongoza kwa ubunifu nchini na tayari imesajili hakimiliki nyingi, ikiwa ni moja ya uthibitisho kuwa teknolojia zinazobuniwa chuoni hapo zinamsaada na zinahitajika sokoni.

Mhe. Chumi pia alihimiza taasisi hiyo kuendelea kushiriki maonesho ya kimataifa ya teknolojia ili kutangaza kazi zao nje ya nchi, huku akiahidi kuwa Wizara ya Mambo ya Nje itaendelea kuwa kiunganishi muhimu kati ya taasisi hiyo na masoko ya kimataifa.

NM-AIST ni taasisi ya elimu ya juu inayolenga kukuza wataalamu wa sayansi na teknolojia barani Afrika, na imekuwa ikihusisha wanafunzi na watafiti kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali barani Afrika.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad