Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, pamoja na mpiga picha wa zamani wa Ikulu, Fredrick Maro, wamekabidhiwa rasmi Vitambulisho vyao vya Uandishi wa Habari (Presscard) leo tarehe 07 Agosti 2025, baada ya kukidhi vigezo vya kisheria vinavyotolewa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).
Zoezi hilo limefanyika katika Ofisi za Bodi zilizopo Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula.
Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi vitambulisho hivyo, Wakili Kipangula alibainisha kuwa Mwambene na Maro wamefuata utaratibu wa kisheria uliowekwa na bodi, ikiwa ni pamoja na kujisajili, kuthibitisha taaluma zao na kuwasilisha vielelezo vinavyotakiwa.“Hili ni zoezi endelevu. Waandishi wote wa habari nchini wanatakiwa kuwa na Presscard inayotolewa na Bodi ya Ithibati ili kuendesha shughuli zao kihalali, kimaadili na kwa mujibu wa sheria,” alisema Kipangula.
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, kifungu cha 19 (1), waandishi wa habari wanapaswa kusajiliwa rasmi na bodi na kuwa na kitambulisho cha kazi kinachotambulika na serikali. Vinginevyo, mtu anayejihusisha na shughuli za uandishi bila kuthibitishwa kisheria anakuwa ametenda kosa.

Assah Mwambene, ambaye pia amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Habari katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, ni mmoja wa waandishi wa habari wenye uzoefu mpana katika sekta ya mawasiliano na diplomasia ya umma. Fredrick Maro naye ni mpiga picha maarufu aliyekuwa karibu na taasisi ya urais kwa miaka kadhaa, na mchango wake umetambuliwa mara nyingi katika vyombo vya habari na kumbukumbu za taifa.
Wakati huo huo, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeendelea na kampeni ya kuwasisitiza waandishi wote wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanasajiliwa, wanathibitishwa, na wanafuata maadili ya taaluma yao.
“Tunapenda kuona tasnia ya habari ikiheshimika, na hilo linaanza na kila mwandishi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Hii inalinda hadhi ya taaluma na maslahi ya umma,” aliongeza Wakili Kipangula.
Mpaka sasa, mamia ya waandishi wa habari wameshasajiliwa na JAB, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na mabadiliko yanayoendelea ndani ya vyombo vya habari na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa ithibati.


No comments:
Post a Comment