HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 11, 2025

Mkutano wa wakuu wa taasisi za umma kuchochea mageuzi na ushindani

 


Dar es Salaam. 
KATIKA  kuendeleza juhudi za Serikali kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa sehemu hai ya uchumi wa kisasa, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa kikao kazi maalum ‘CEO Forum 2025’ kitakachowaleta pamoja Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa mashirika ya umma nchini wapatao 700.

Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 23-26 jijini Arusha, unalenga kujadili kwa kina jinsi taasisi za umma zinavyoweza kuwa shindani katika soko la kimataifa, kuongeza mapato yasiyo ya kodi, na kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa kisasa unaoongozwa na matokeo.

Kupitia mijadala ya kitaasisi, Serikali inalenga kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na ubunifu katika taasisi hizi ili ziweze kuwa wabia halisi wa maendeleo ya Taifa.

Aidha, akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatatu, Agosti 11, 2025, Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini---Mashirika ya Umma ya kibiashara, alisema kipaumbele kitawekwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050, kwa kuhakikisha taasisi za umma zinajipanga kuwa wabia wa kweli wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Dira 2050, Serikali imedhamiria kuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, huku pato la Taifa likifikia $1 trilioni na pato la mtu mmoja mmoja $7000 kwa mwaka.

Bi. Mauki alisema ili kufikia matamanio hayo ni lazima kujenga misingi imara ya ushirikiano kati ya vyombo vya maamuzi na wasimamizi wa utekelezaji ndani ya taasisi za umma, ili kuongeza tija, uwajibikaji na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kikanda na kimataifa.

Ni katika muktadha huo, katika kipindi ambacho dunia inakumbwa na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi, kiteknolojia na kisera, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imetambua haja ya kuwa na jukwaa mahsusi la kujadili, kutathmini na kuimarisha mwelekeo wa pamoja wa taasisi zake za umma – ndipo likazaliwa wazo la CEO Forum miaka mitatu iliyopita.

“Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inaendelea kuimarisha juhudi za mageuzi ndani ya taasisi za umma kwa kuandaa kikao kazi maalum – CEO Forum 2025 – ambacho kitawakutanisha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wapatao 700 wa taasisi zote za umma nchini,” alisema Bi. Mauki.

Aliongeza: “Lengo letu kuu ni kutathmini kwa pamoja nafasi ya taasisi za umma katika uchumi wa sasa unaobadilika kwa kasi na kuhitaji mifumo shindani, bunifu na yenye uwajibikaji wa juu.

Bi. Mauki alisema kwa mazingira hayo, watatumia mkutano huo kama jukwaa la kimkakati linalolenga kuimarisha mawasiliano, mshikamano wa kiutendaji, na kuweka dira ya pamoja kati ya bodi na menejimenti za taasisi za umma.

Alieleza kuwa mkutano huo si tu mkutano wa kawaida, bali ni sehemu ya mwendelezo wa mageuzi yanayolenga kuongeza mchango wa mashirika ya umma katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

“Tunatarajia majadiliano ya kina kuhusu namna taasisi zetu zinaweza kuwa shindani katika soko la kimataifa, ziweze kuongeza mapato yasiyo ya kodi, na kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa kisasa,” alisema Bi. Mauki.

Aliongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara Katika Mazingira Shindani Kimataifa – Nafasi ya Mashirika ya Umma,” inaonyesha wazi kwamba taasisi za umma haziwezi tena kujiendesha kwa mifumo ya zamani, bali zinahitaji mwelekeo mpya wa kibiashara, ushirikiano na ufanisi wa hali ya juu.

Katika kikao hicho, washiriki wanatarajiwa kujadili changamoto, fursa na mikakati ya mageuzi yenye kuleta matokeo.

Bi. Mauki ameweka bayana kuwa matarajio ya Serikali ni kuona mkutano huo unaleta matokeo, ikiwa ni pamoja na kubuni mifumo mipya ya usimamizi, kuimarisha maadili ya kiuongozi, na kujenga mazingira ya kazi yanayowezesha uwajibikaji na ubunifu.

Aliongeza kuwa kikao hicho pia kitaleta fursa ya kujifunza kutoka kwa taasisi zilizopiga hatua, na hivyo kutoa mwanga kwa zile zinazokabiliwa na changamoto.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad