HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 7, 2025

Mkurugenzi Mkuu wa PURA Apongeza TPDC kwa Mchango wa Gesi Asilia katika Maendeleo ya Kiuchumi





📍Dodoma, Agosti 7, 2025
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, ametembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, na kujionea teknolojia mbalimbali za usimamizi na usambazaji wa gesi asilia zinazotekelezwa na TPDC kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhandisi Sangweni alieleza kuwa kugundulika kwa gesi asilia nchini kumeleta manufaa makubwa kwa wananchi, hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, usafirishaji na matumizi ya nyumbani, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

“Gesi asilia, ambayo kimsingi ni Methane (CH₄), inachangia uzalishaji wa mbolea ya Ammonium Sulphate au Ammonium Phosphate kupitia kiwanda maalum kinachotenganisha na kutengeneza Ammonium. Mbolea hii ni muhimu katika kuongeza tija mashambani,” alifafanua kitaalamu.

Aidha, Mhandisi Sangweni alieleza kuwa matumizi ya gesi kwenye vyombo vya moto yana faida kubwa kwani husaidia kupunguza gharama za matengenezo kutokana na ufanisi wake wa kiufundi.

“Mfumo wa gesi unapunguza hitaji la kutumia mafuta ya petroli mara kwa mara, na hivyo huchochea muda mrefu wa huduma kwa vifaa kama vile fuel pump, filters na hata spark plugs; ambazo hazichafuki kwa haraka,” aliongeza.

Alisifu jitihada za TPDC katika kupanua miundombinu ya gesi nchini, ikiwemo ujenzi wa mtandao wa usambazaji gesi asilia jijini Dodoma pamoja na uwepo wa vituo vya gesi vya muda (mobile gas stations) katika jiji hilo.

“Kwa kutumia gesi, gari linaweza kusafiri zaidi ya kilomita 40 kwa kiasi kilekile cha mafuta ambacho kingesafiri kilomita 10 tu kwa petroli. Kwa bajaji, unaweza kwenda zaidi ya kilomita 60 badala ya 30. Huu ni unafuu mkubwa kwa wananchi,” alisisitiza.

Mtaalamu huyo kutoka PURA alihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika matumizi ya gesi kwa shughuli za kupikia na usafiri ili kuokoa gharama, kulinda mazingira na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Mwisho, alitoa pongezi kwa uongozi wa wizara chini ya Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko, Bodi ya TPDC na Serikali kwa ujumla kwa kuendeleza usimamizi madhubuti wa sekta ya gesi nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad