Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Katika kuunga juhudi za kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii nchini, kampuni ya utalii ya Meru Eco Camp imezindua mkakati kabambe wa maboresho ya huduma unaolenga kuvutia wageni wa ndani na nje ya Tanzania.
Kampuni hiyo inayotoa huduma ndani ya Hifadhi ya Shamba la Miti la Meru, wilayani Arumeru mkoani Arusha, sasa inajivunia kuwa na vivutio vya kipekee vikiwemo maporomoko ya maji ya Napuru (Napuru Waterfalls), malazi ya kisasa na rafiki kwa mazingira, pamoja na michezo ya kusisimua ikiwemo zipline yenye urefu wa mita 800 – zipline ndefu zaidi Afrika Mashariki – inayokatiza kutoka msituni hadi mto Themi uliopo katikati ya jiji la Arusha.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Utalii, Mkurugenzi Mtendaji wa Meru Eco Camp, Catherine Loy, alisema:
“Tumejipanga kuifanya Meru Eco Camp kuwa kitovu cha utalii wa asili na burudani kwa wageni wote. Tunaongeza michezo ya kipekee kama gofu, kurusha mishale, baiskeli, na pikipiki kwa ajili ya watalii wanaopenda kujichanganya na mazingira.”
Kwa upande wake, Nsajigwa Victor, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alieleza kuwa wanatarajia kujenga eco lodges – malazi ya kiasili yanayozingatia utunzaji wa mazingira – ili kuongeza idadi ya watalii wanaolala hifadhini.
Lucas Christopher, mtaalamu wa masuala ya fedha wa Meru Eco Camp, alisema maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana na kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa kupitia utalii endelevu.
Naye Colins James, Mkurugenzi Msaidizi wa New Meru Camp, aliongeza kuwa mbali na malazi, wameandaa michezo mingi ya kuvutia, hasa kwa familia na vijana, ikiwa ni sehemu ya kuvutia wageni wapenda burudani za mazingira.
Kwa upande wake, Fredy Msaki, Mratibu wa kampuni ya utalii ya FOCA, alibainisha kuwa kuna programu maalum za malazi kwa bei nafuu kwa familia na watalii wote watakaotembelea Hifadhi ya Shamba la Miti la Meru.
Mpango huu mkubwa unatajwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya Arusha kuendelea kuwa kitovu cha utalii Afrika Mashariki huku ukiibua matumaini mapya kwa jamii inayozunguka msitu wa Meru.
Eneo la Malazi ya kisasa...
Zipline... Moja ya mchezo unaopendwa na Watalii.
Eneo la Maporomoko ya Maji ya Napuru
No comments:
Post a Comment