MADAKTARI bingwa wa saratani, wataalamu wa tiba mionzi, watafiti, watunga sera pamoja na mashujaa wa saratani kutoka kwenye nchi zaidi ya 20 wanatarajiwa kushiriki kongamano la kwanza la kimataifa la saratani linalotarajiwa kufanyika hapa nchini.
Aidha zaidi ya washiriki 600 wakiwemo washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi wanatarajiwa pia kushiriki katika kongamano hilo ambalo ni sehemu ya kuadhimisha miaka 30 ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) katika kutoa huduma tangu kuanzishwa kwake.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Diwani Msemo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo ambapo amesema linatarajiwa kufanyika Februari 4 hadi 6, 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.
Dk. Msemo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo amesema kwa pamoja washiriki hao watatafakari safari ya taasisi hiyo katika kipindi chote cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kushirikishana ubunifu na kupanga njia bora zaidi ya kudhibiti saratani nchini Tanzania na kwingineko.
“Maadhimisho haya yatatanguliwa na shughuli mbalimbali ambazo zitaanza mnamo mwezi Januari 2026 ikiwa ni pamoja na majukwaa mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti kuhusiana na saratani, tutafanya vipindi katika vyombo vya habari ambavyo vitahusu elimu kuhusu saratani,” amesema Dk. Msemo na kuongeza.
“Siku mbili za mwanzo yaani Februari 4 hadi 5, 2026 zitakuwa ni za kongamano hili la kwanza la kimataifa la saratani na Februari 6, 2026 itakuwa ni kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 30 ya taasisi yetu ya saratani,” amesema
Aidha amesema tangu kuanzishwa kwa ORCI, imekuwa taa ya matumaini kwa wagonjwa wa saratani nchini, ikitoa huduma kamili ikiwemo tiba ya mionzi, tiba ya dawa (chemotherapy), upasuaji wa saratani, tiba ya nyuklia, uchunguzi wa saratani, utafiti, mafunzo na huduma za kupunguza maumivu.
“Katika miongo hii mitatu tumegusa maisha ya wengi, kujenga timu ya wataalamu mahiri na kufanikiwa kujenga mahusiano muhimu katika nyanja hii ndani ya taifa na hata kimataifa,” amesema
Hata hivyo amesema kuelekea kwenye tukio hilo watahakikisha wanatambua na kuthamini michango ya watumishi na wafanyakazi wa taasisi hiyo kutoka kuanzishwa kwake, mashujaa wa saratani, washiriki na wafadhili.
“Pia tutaongeza uelewa wa umma kuhusu kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu sahihi ya saratani na maudhi madogo madogo yatokanayo na matibabu ya saratani, tutazindua mpango mkakati wa 2026-20230 wenye lengo la kupunguza vifo vya saratani kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030,” amesema
Amesema kwa kutumia vifaa vya kisasa ikiwemo mashine ya kisasa ya kugundua saratani iliyojificha kwa njia ya nyuklia, utaalamu wa hali ya juu na huduma zenye ubora watawakaribisha wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaotafuta matibabu bora ya saratani kwa gharama nafuu na kwa mazingira yenye utu na heshima.
“Sambamba hayo mengine tumezindua tovuti ramsi kwa ajili ya maadhimisho haya ya miaka 30, watanzania tunawahimiza kuitembelea, kufahamu huduma na kuitumia kama Daraja la kuunganishwa nasi,” amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Tiba Utalii kutoka Wizara ya Afya, Dk. Asha Mahita amesema saratani duniani zinazoongoza ni ya mlango wa kizazi na matiti kwa kina mama, tezi dume kwa kinababa na saratani ya koo na nyinginezo.
“Hivyo tunamkakati wa kuelimisha jamii yetu ya nje na ndani katika kukinga haya magonjwa, hivyo katika kongamano hilo tutakuwa na mada tofauti tofauti kwa lengo la kuelimisha jamii kwani kati ya watu 100,000 wanaokuja kupima 68,000 wanakutwa na viashiria vya saratani,” amesema
No comments:
Post a Comment