-Asema REA inabeba kikamilifu ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia
-Ampongeza Mwenyekiti wa Bodi (REB) na Mkurugenzi Mkuu REA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kukamilisha lengo la usambazaji Umeme katika Vijiji 12,318 Nchini na kwa umahiri wake katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Ametoa pongezi hizo Agosti 22, 2025 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia Nishati Safi kwa Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“REA mmefanya kazi kubwa, tunawapongeza kwa kuibeba vyema ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Nishati Safi ya Kupikia sambamba na kukamilisha kwa wakati lengo la kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 na sasa mnasambaza umeme vitongojini,” alipongeza Mhe. Dkt.Biteko.
Aliongeza kuwa miradi yote inayosimamiwa na REA inakamilika kwa wakati na kwa ubora mzuri na kwamba hajawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wafadhili wa miradi na mara zote wamekuwa wakimpatia sifa njema za utendaji wa Wakala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alisema Wakala unaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo na alipendekeza taasisi zingine nazo ziweke utaratibu wa kugawa Nishati safi kwa watumishi wake.
“Ombi langu zoezi hili itapendeza na kuleta matokeo chanya endapo taasisi zote zitatoa majiko haya kwa watumishi; hii italeta chachu kwa Wizara zingine na taasisi mbalimbali kufanya vivyo hivyo na itaongeza kasi ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya kuhakikisha 80% ya Watanzania wanahamia kutumia Nishati Safi ifikapo mwaka 2034 na hili linawezekana,” alisema Balozi Kingu.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy aliainisha mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kupitia REA na alitaja baadhi ya miradi ikiwemo mradi wa kujenga mifumo ya gesi asilia Lindi na Pwani na kwamba hadi sasa wananchi 460 wamefikiwa kati ya 980 waliolengwa, kufunga mifumo katika Jeshi la Magereza ambapo magereza yote 129 yamefikiwa sambamba na kufunga mifumo katika kambi 22 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).














No comments:
Post a Comment