NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Charles Shirima,amesema uwekezaji katika kampuni za umma umeongezeka kwa kiwango cha juu tofauti na awali.
Ameeleza hayo wakati akizungumza na wananchi pamoja na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya nanenane yanayofanyika Dodoma, kwa kubainisha kuwa wamekuja kutoa fursa kwa wananchi na wakulima wa kanda ya kati kujifunza kuhusu soko la mitaji na sekta ya soko la bidhaa ambalo wanaweza kuuza mazao kwa ushindani.
“CMSA kazi yetu ni kuratibu na kusimamia shughuli za uendeshaji na usimamizi wa biashara katika soko la hisa na fursa za uwekezaji katika hisa za kampuni, hati fungani ambazo umma unaweza kuwekeza akiba kwa njia endelevu.
Mfumo huu pia unawezesha biashara mbalimbali ambapo serikali inaweza kukusanya mtaji kupitia umma unaowekeza katika Nyanja mbalimbali za uchumi wa mtu mmoja mmoja na umma.”
Alibainisha kuwa mwitikio ni mzuri na wawekezaji katika soko la mitaji ya umma wameongezeka, akitolea mfano ushiriki wa mifuko ya uwekezaji kuwa mkubwa.
“Mwanzoni tulikuwa na mfuko mmoja tu wa UTT-AMIS kwa sasa umeongezeka pia ushiriki katika hati fungani za serikali katika kampuni na mwitikio umekuwa mkubwa.”
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Elimu kwa umma CMSA, Stella Anastazi, alisema mamlaka hiyo imewezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni na wameanzisha mfumo wa soko la bidhaa ili kutoa fursa kwa wakulima kupata masoko ndani na nje ya nchi.
Naye, Christopher Ngonyani kutoka CMSA, alisema uwekezaji huo umetoa fursa kwa watu kujipatia gawio na kuwepo ongezeko la thamani la uwekezaji wao huku akitoa rai kwa wananchi wasiowekeza kufanya hivyo.
“Moja ya changamoto ni ushiriki mdogo wa watanzania kuwekeza kwenye vipande hivyo tunatoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuwekeza,”ameeleza.
No comments:
Post a Comment