HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 23, 2025

WANANCHI WAHIMIZWA KULINDA MIUNDOMBINU YA ELIMU IRINGA-RC KHERI

Kwa kutambua kazi iliyofanywa na serikali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Kheri James amewahimiza wananchi Mkoani humo kuhakikisha wanalinda na kuitunza miundombinu iliyojengwa katika sekta ya elimu mkoani humo ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kuufikisha mkoa katika lengo la kuinufaisha jamii kielimu na taifa kwa ujumla.

Ametoa rai hiyo wakati akizungumzia hatua zilizofikiwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia Mradi wa kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).

Mhe Kheri amesema kuwa Mkoa wa Iringa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 umepokea kiasi cha shilingi 21,017,700,420.

Amesema fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Shule za Sekondari. Aidha, miundombinu iliyojengwa katika kipindi hicho ni pamoja na Shule mpya za kata, Shule ya wasichana ya Mkoa (Lugalo), Shule ya amali Mafinga, Mabweni, Madarasa, nyumba za walimu pamoja na matundu ya vyoo.

"Serikali imejenga Shule mpya 24 ambapo kabla ya kujengwa kwa Shule hizi wanafunzi wengi walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari jambo lililohatarisha usalama wa wanafunzi hususani watoto wa kike na wengine walikata tamaa na kushindwa kuendelea na masomo yao, Lakini sasa wanafunzi wamepata fursa ya kusoma katika shule hizi ambazo zimejengwa katika maeneo yao" Amekaririwa Mhe Kheri

Ameongeza kuwa Serikali imejenga mabweni 44 ndani Mkoa wa Iringa ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya malazi ya wanafunzi wa kike na wa kiume, Vilevile Imejenga nyumba 11 (two in 1) kwa ajili ya walimu.

"Pia Serikali imeleta vitabu vya kuifundishia kwa shule za Msingi na sekondari na kuajiri walimu wa shule za Msingi na Sekondari na kuwajengea uwezo wa mbinu za kisasa za ufundishaji kwa njia ya TEHAMA, na imeleta vifaa vya maabara na vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya shule za sekondari na vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu" Amesisitiza Rc Kheri

Amesema kuwa maelengo ya serikali ya awamu ya sita ni Kuongeza fursa ya upatikanaji wa Elimu ya Sekondari, Kuweka mazingira salama ya Elimu kwa wasichana waliopo katika shule za sekondari, Kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoanza masomo ya Sekondari (wanakamilisha mzunguko) au kumaliza Elimu ya Sekondari.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad