HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 21, 2025

TAMISEMI yawanoa Maafisa Tarafa na Watendaji wa kata 200 kuzingatia Sheria na Miongozo

Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa wito kwa watendaji wa Malaka za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali katika kuwahudumia wananchi ili kuondoa migogoro ya kiutendaji kati ya wataalam na Viongozi wa maeneo husika.

Wito huo umetolewa leo Julai 21, 2025 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila kwa niaba ya Katibu Mkuu Adolf Ndunguru wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wapya kutoka Mikoa ya Tabora, Singida, Iringa, Morogoro na Dodoma walioajiriwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.

Mhandisi Mativila amesema miongoni mwa sababu zilizo ongeza msukumo wa kuandaliwa kwa mafunzo hayo ni usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo, kutotatuliwa kwa wakati kwa kero za wananchi, kukosekana kwa ubunifu katika usimamizi wa fursa za maendeleo, changamoto za kimaadili kwa baadhi ya watumishi pamoja na Uelewa mdogo wa sera, sheria na miongozo ya Serikali.

“Baada ya ushiriki wenu katika mafunzo haya OR – TAMISEMI inaamini mtaenda kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, uadilifu, uwajibikaji, na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na maadili ya utumishi wa umma” alisisitiza Mhandisi Mativila

Mafunzo hayo yaliyobuniwa mahususi kuwawezesha watumishi wapya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi yakiwa yameandaliwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) pamoja na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), yakilenga kukabiliana na changamoto zilizobainika kutokana na uzoefu wa kiutendaji ambazo zimeathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi katika ngazi ya Tarafa na Kata.

Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na wanazostahili Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa kushirikiana na vyuo vya LGTI na TPSC, tayari imetoa mafunzo kwa Maafisa Tarafa 538 na Watendaji wa Kata 3,948 wa Tanzania Bara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 hadi 2023/24, yakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2011 kuhusu Mafunzo Elekezi kwa Watumishi wa Umma.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad