Na Mwandishi Wetu, Michuzi Blog
WAKULIMA katika wilaya za Kondoa na Chemba wanaendelea kupewa mafunzo ya stadi na ujuzi wa ujasiriamali kwa lengo la kuwawezesha kuwa na vyanzo mbalimbali vya kipato badala ya kutegemea kilimo pekee.
Hatua hiyo inalenga pia kuhakikisha kuwa wakulima wanaongeza thamani kwenye mazao yao ya kilimo kama vile alizeti, karanga na mtama, ambayo ni rahisi kuchakatwa.
INADES-Formation Tanzania (IFTz), kupitia ufadhili wa Shirika la Kijerumani la Bread for the World (BftW), imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wakulima katika vijiji vya mradi wilayani Chemba na Kondoa, ili kuhakikisha wanajikita katika biashara ya kilimo.
Afisa Mradi wa IFTz anayeshughulikia Afya ya Jamii na Masuala ya Jinsia, Bw. Rajabu Rajabu, alisema hivi karibuni wakati wa mafunzo kwa wakulima katika kijiji cha Potea wilayani Kondoa kuwa stadi za ujasiriamali ni muhimu endapo wakulima wanataka kuongeza kipato kutokana na mazao yao.
Alisema kupitia vikundi vya Vicoba (Village Savings and Loans – VSL), IFTz inatoa mafunzo ya ujasiriamali yanayohusisha shughuli za kilimo na zisizo za kilimo ili kuwawezesha wakulima kuwa na vyanzo mbadala vya kipato.
“IFTz imekuwa ikifundisha wakulima katika vijiji vya mradi kuhusu stadi mbalimbali za ujasiriamali. Leo tumewapa mafunzo ya kutengeneza mafuta ya mwili na kiwi ya viatu kwa kutumia mafuta ya kupikia, rangi, manukato kidogo na mafuta ya custard,” alisema.
Kwa mujibu wake, programu hizo zina hakikisha wakulima wanatumia malighafi zinazopatikana kijijini ili kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo. Mafunzo hayo yanatolewa katika vijiji vya Sambwa, Waida, Mauno, Keikei, Daki, Isini na Sarare wilayani Kondoa na Chemba.
Halima Nyeresa, mwezeshaji wa ujasiriamali katika tukio hilo, alisema kuwa kupata mafunzo kutoka kwa mashirika mbalimbali kama IFTz na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kumemuwezesha kuongeza kipato, kuwasomesha watoto wake vyuo vikuu na kutimiza mahitaji ya kila siku.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Amina Lungi, alisema kuwa stadi na maarifa aliyojifunza katika mafunzo ya ujasiriamali ni muhimu katika kuboresha maisha yao, kuongeza kipato na kuwawezesha kuishi maisha bora yenye afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa INADES-Formation, Bw. Mbarwa Kivuyo, alisema kuwa shirika lake linaamini kuwa kilimo ni biashara, hivyo kuwapa wakulima mafunzo ya ujasiriamali ni kuwaandaa kuuza mazao yao kwa faida.
“Mfanyabiashara yeyote ni lazima ajue kutofautisha mtaji na faida. Anapaswa kujua namna ya kufanya hesabu kabla ya kuwekeza katika uzalishaji. Mafunzo yetu yanawapa wakulima uwezo wa kubaini fursa zilizopo kwenye kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa shughuli za shirika lake zinajengwa juu ya msingi wa kutoa mafunzo ya uongozi na kilimo kwa wakulima pamoja na kuhakikisha wanapata wanunuzi wa mazao yao, hasa yale yaliyolimwa kwa njia ya kiikolojia au kilimo hai. Alisisitiza umuhimu wa wakulima kuzalisha kwa ubora na wingi unaohitajika na soko.
.jpeg)
No comments:
Post a Comment