HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 23, 2025

NAIBU KATIBU MKUU (ELIMU) WyEST AFANYA ZIARA TLSB

 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohamed Omar ametembelea Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Makao Makuu Dar es Salaam leo tarehe 22 Julai, 2025 kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Bodi ikiwa ni takribani mwezi mmoja sasa tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.

Dkt. Omar, amesema lengo la ziara hiyo ni kuifahamu TLSB na shughuli zake huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi kwa hatua iliyofikia kuelekea utoaji wa huduma za Maktaba kwa njia ya Mtandao kupitia Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa ambayo iko mbioni kuzinduliwa.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Bodi na Menejimenti kwa hatua mliyofikia kuelekea kutoa huduma za Maktaba kidijitali, hatua hii itawezesha wananchi walio wengi hasa waishio pembezoni mwa miji kupata huduma za maktaba kwa urahisi na kuchochea utamaduni wa kujisomea na kujipatia maarifa” amesema Dkt. Omar.

Sambamba na hilo, ameongeza kuwa atafanya jitihada za kutafuta washirika na miradi itakayowezesha Watumishi wa Bodi kwenda kujifunza nje ya nchi masuala ya Maktaba kwa teknolojia za kisasa ili kutekeleza shughuli za Bodi kwa viwango vya kimataifa kama zilivyo maktaba nyingi za ughaibuni.

Awali katika taarifa yake kuhusu Bodi, majukumu na shughuli inazotekeleza, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, alieleza pia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne (2021 -2025), huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimairisha miundombinu ya maktaba kwa kujenga na kukarabati majengo ya maktaba nchini, uanzishaji wa Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa, ununzi wa vifaa vya TEHAMA, maboresho ya sheria, ongezeko la Bajeti, ongezeko la Watumishi kupitia ajira mpya na mradi wa ununuzi wa Vitabu vitakazosambazwa kwenye Maktaba za jamii ili kuzidi kupeleka maarifa na kuongeza ari ya usomaji hasa kwa watoto na vijana. 

Dkt. Ruzegea amezungumzia pia maboresho yaliyofanyika katika Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) kwa kuongeza kozi mbili mpya ambazo ni; TEHAMA (ICT) na Uongozi wa Biashara (Business Management) kwa ngazi ya Stashahada (Diploma) katika Mitaala yake iliyoboreshwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala (WyEST) ndug. Sebastian Enoshi, aliyeambatana na Naibu katibu Mkuu, amemuelezea Dkt. Omar kwamba si mgeni katika uongozi, kwani ametokea Wizara ya Kilimo, lakini kwasasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona ni vyema amhamishie Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusukuma gurudumu la Elimu na kuwataka Watumishi wa Bodi kumpa ushirikiano.

Hapo awali akiwasili katika ofisi za TLSB, Dkt. Omar, alitembelea divisheni mbalimbali za Bodi zikiwemo; Divisheni ya Usomaji ya Watu Wazima, Divisheni ya Watoto na Shule, Kitengo cha Ufundi na Kitengo cha Bibliografia ya Taifa na kupata maelezo kwa kina kuhusu divisheni na vitengo hivyo vinavyotekeleza majukumu yake.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu alipata wasaa wa kukutana na Watumishi wa TLSB Makao Makuu na Watumishi wa Chuo cha SLADS katika kikao maalum kilichofanyika katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano TLSB ambapo Watumishi wa TLSB mikoani walifuatilia kikao hicho kwa njia ya mtandao.
 NaiKatibu Mkuu (ELIMU) wa WyEST Dkt. Hussein Mohamed Omar (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea (Kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala (WyEST) ndug. Sebastian Enoshi (Kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya TLSB leo tarehe 22 Julai, 2025 mara baada ya kutamatika kikao cha Naibu Katibu Mkuu na Watumishi wa TLSB.




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad