HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 23, 2025

Bodi ya Ithibati Yakabidhi Press Card kwa Kiongozi wa Michuzi Media

 

●Waandishi Wengine Watakiwa Kuhakiki Viambatisho Katika Mfumo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amemkabidhi rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Card) Mkurugenzi Mtendaji wa Michuzi Media Group, Muhidin Issa Michuzi, kwa niaba ya waandishi wengine wanaoendelea kukamilisha taratibu za kupata vitambulisho hivyo.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la Bodi hiyo katika kuhakikisha kuwa waandishi wote nchini wanakuwa na vitambulisho halali kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.

Akizungumza baada ya kukabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula amempongeza Michuzi pamoja na waandishi wengine waliokwishapatiwa vitambulisho vyao kwa kufuata taratibu na kukidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.

Amesisitiza kuwa mchakato wa utoaji wa vitambulisho bado unaendelea na ametoa wito kwa waandishi ambao maombi yao hayajakamilika kuingia katika mfumo rasmi wa Bodi ili kuhakiki viambatisho walivyowasilisha.

“Kuna baadhi ya waombaji ambao viambatisho vyao havifunguki, havisomeki, vimerudiwa au havikidhi matakwa ya kisheria kama vile vyeti visivyotambulika au kukosekana kwa barua za utambulisho kutoka kwa waajiri,” amesema Wakili Kipangula.

Ametoa rai kwa waandishi kuhakikisha wanafuata maelekezo yanayotolewa kupitia mfumo kabla ya kuwasiliana moja kwa moja na Bodi kuhusu hali ya maombi yao.
JAB imekuwa ikitekeleza jukumu la kuthibitisha na kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanahabari wanatambulika rasmi na kuwa na vitambulisho halali vinavyotolewa kwa mujibu wa sheria.

Michuzi ameishukuru Bodi kwa mchakato huo na kuwataka waandishi wengine kuhakikisha wanazingatia taratibu ili kuimarisha tasnia ya habari kwa weledi na uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad