HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 17, 2025

WAZIRI SIMBACHAWENE AIPONGEZA TCAA KWA UTENDAJI BORA KATIKA MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2025

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi na mchango wake katika kukuza maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.

Waziri Simbachawene alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TCAA katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, Dodoma, ambapo pia alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo kwa mwaka 2025.

Katika ziara hiyo, Waziri Simbachawene alipokelewa na maafisa wa TCAA na kuelezwa kuhusu majukumu ya msingi ya Mamlaka hiyo, yakiwemo usimamizi wa usalama wa anga, huduma ya uongozaji ndege, utoaji wa leseni za usafiri wa anga, pamoja na kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano ya uhakika baina ya marubani na waongozaji ndege kupitia mifumo ya kisasa ya mawasiliano ya sauti ‘VHF’.

Aidha, Mhe. Simbachawene alifahamishwa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na TCAA, ikiwemo mradi wa uboreshaji wa mitambo ya mawasiliano ya sauti na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), kinachotarajiwa kuwa kitovu cha mafunzo ya anga kwa Afrika Mashariki.

“Ni jambo la kujivunia kuona taasisi kama TCAA zikitekeleza majukumu yake kwa weledi na kuendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha huduma kwa wananchi na kukuza maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Simbachawene.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Utoaji wa Huduma kwa Wananchi: Dhamira ya Mabadiliko ya Kiutawala Barani Afrika”, yakilenga kuhamasisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma zenye tija katika taasisi za umma. TCAA ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kikamilifu kuonesha mafanikio na huduma zake kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza alipotembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mtoa Taarifa za Anga Daudi Mziray (katikati) kuhusu utekelezaji wa mradi wa Mawasiliano pamoja na chuo cha usafiri wa anga (CATC) alipotembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Habari na Mawasiliano wa TCAA Maureen Swai.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Mtoa Taarifa za Anga Daudi Mziray (katikati) aliyekabidhi kwa niaba ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Habari na Mawasiliano wa TCAA Maureen Swai.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad