Na Mwandishi wetu
MCHEZAJI wa gofu kutoka klabu ya Lugalo jijini Dar es Saalam, Meja Chediel Msechu amewataka waandaaji wa mashindano ya Lina PG Tour kuendelea kuandaa michuano hiyo ambayo ina lengo la kukuza vipaji katika mchezo wa gofu nchini.
Meja Msechu ameyasema hayo jana wakati wa mashindano ya Lina PG Tour msimu wa tatu yaliyorindima katika Viwanja vya TPC Moshi mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani timu ya Taifa ya wanawake marehemu Lina Nkya.
Alisema Lina PG Tour ni mashindano mazuri yaliyoandaliwa kwa weledi mkubwa hivyo anawapongeza wandaaji wote na kuwaomba waendelee kuyaandaa ili kuweza kupata na kukuza vipaji vya wachezaji katika mchezo wa gofu.
“Nafarijika sana kuyaona mashindano haya ambayo yamekuwa chachu kubwa katika maendeleo ya mchezo wa gofu yanafanyika kwa weledi na mpangilio mzuri, niwapongeza waandaaji kwa kazi kubwa wanayofanya na niwaombe wasivunjike moyo bali waendelee kuhakikisha mashindano yanakuwepo ili kukuza vipaji katika mchezo huu,” alisema
Meja Msechu amesisitiza kuwa Lina PG Tour imekuwa ikitoa changamoto kwa wachezaji wakubwa hasa wale wa kulipwa kuweza kushindana ili kupata nafasi ya kwenda kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa nje ya nchi.
Naye Mchezaji wa gofu kutoka klabu ya Kilimanjaro, Rachel Mushi alisema kupitia mchezo huo wa gofu aliweza kupanda ndege kwa mara ya kwanza, kukutana na kufahamiana na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment