Mtendaji Mkuu wa TIC, Gilead Teri akiwaonesha aandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 9, 2025 mabango ya jinsi uwekezaji na ajira zinavyokuwa katika miradi mbalimbali kuaanzia Januari hadi Mei, 2025.
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili miradi ya uwekezaji 372 katika kipindi cha Januari hadi Mei 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.04 ikilinganishwa na miradi 335 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za mikoa kadhaa ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuvutia wawekezaji.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa TIC, Gilead Teri, mikoa iliyoongoza kwa usajili wa miradi ni Dar es Salaam kwa miradi 134, ikifuatiwa na Pwani yenye miradi 90, Arusha miradi 29, Dodoma miradi 14, na mikoa ya Geita na Morogoro ambayo kila moja imesajili miradi 13.
Mikoa hii sita imekuwa mhimili mkuu wa mafanikio ya TIC katika kipindi hiki, ikichangia zaidi ya nusu ya miradi yote iliyosajiliwa nchini. Dar es Salaam na Pwani pekee zimechangia karibu asilimia 60 ya miradi yote kwa pamoja, jambo linaloonesha nguvu kubwa ya kiuchumi na mazingira rafiki ya uwekezaji katika ukanda wa mashariki mwa nchi.
Aidha, Teri ameeleza kuwa miradi hiyo kwa ujumla wake ina thamani ya Dola za Marekani milioni 3,755.4, sawa na ongezeko la asilimia 31.9 ikilinganishwa na Dola milioni 2,847.6 kwa kipindi kama hicho mwaka jana. Miradi hiyo inatarajiwa kuleta ajira mpya 41,117 kwa Watanzania.
Katika kuongeza mwitikio wa ndani, TIC imetekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha chini cha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani kutoka Dola 100,000 hadi 50,000, kuanzishwa kwa ofisi ya Kanda ya Nyasa (Njombe), na kuimarishwa kwa huduma kupitia Kituo cha Huduma Maalumu kwa Wawekezaji (PISC).
Kwa upande wa sekta, Viwanda vimeongoza kwa miradi 156, Usafirishaji 56, Kilimo 40, Utalii 39 na Ujenzi wa Majengo ya Biashara miradi 36. Hii inaonyesha kuwa mikoa kama Dar es Salaam, Pwani na Arusha imeendelea kunufaika na uwekezaji katika sekta hizi kutokana na miundombinu bora na vivutio vya kiuchumi vilivyopo.
Teri amesema TIC inalenga kusajili miradi 1,500 kwa mwaka 2025, huku mkazo ukiwekwa kwenye huduma za Aftercare kwa wawekezaji waliopo, kutatua changamoto zao, na kuhimiza miradi ya upanuzi. Tayari, miradi 32 ya upanuzi imesajiliwa katika kipindi hiki, ikilinganishwa na 21 kwa mwaka 2024.
Kwa kumalizia, TIC inatoa wito kwa mikoa mingine kuongeza juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwa kushirikiana na TIC, ili kufikia malengo ya kitaifa ya kukuza uchumi jumuishi unaomshirikisha Mtanzania kupitia miradi ya ndani na ya ubia.
Matukio mbalimbali katika picha.
No comments:
Post a Comment