SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wadau wa mnyororo wa thamani wa chakula kuanzia wakulima shambani, viwandani, wafanyabiashara hadi watumiaji wa mwisho kuhakikisha kuwa chakula kinachoingia sokoni ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Wito huo umetolewa leo Juni 6, 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Meneja Uchanganuzi wa Hatari Zitokanazo na Chakula (TBS), Bi. Immakulatha Justin, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 7.
Bi. Immakulata amesema suala la usalama wa chakula ni mtambuka, likihusisha hatua zote za uzalishaji hadi mlaji wa mwisho, hivyo linahitaji ufuatiliaji na uwajibikaji wa hali ya juu ili kuzuia athari zinazoweza kuzuilika.
“Kule shambani, wazalishaji hutumia pembejeo mbalimbali kama vile dawa za kuua wadudu. Ni muhimu dawa hizi zitumike kwa kufuata maelekezo ya wataalamu ili zisije kuathiri usalama wa chakula,” amesema Bi. Immakulata.
Aidha, amewahimiza walaji kuhakikisha wanachunguza chakula wanachonunua ili kubaini kama kuna viashiria vya uchafuzi kabla ya kukitumia, hatua itakayosaidia kuepuka athari za kiafya.
Kwa upande wa wafanyabiashara, amewaasa kuzingatia ubora na usalama wa chakula wanachouza badala ya kuangalia bei peke yake, pamoja na kuhifadhi chakula katika mazingira safi na salama.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani mwaka huu yanafanyika kwa mara ya saba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, na yanabeba kaulimbiu: "Chakula Salama: Sayansi Katika Vitendo"
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha matumizi ya sayansi na mbinu bora kuhakikisha chakula kinachowafikia walaji ni salama.



No comments:
Post a Comment