HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 25, 2025

Tanzania Yaungana na Msumbiji Kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru, Ushirikiano wa Kihistoria Waangaziwa











Maputo, Msumbiji – Juni 25, 2025
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameungana na wananchi wa Msumbiji kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika, akisisitiza mshikamano wa kihistoria na undugu usiotenganishwa na mipaka wala mito.

Akihutubia hadhira iliyojumuisha Marais wa zamani wa Msumbiji, viongozi wa Afrika na maelfu ya wananchi wa Msumbiji katika Uwanja wa Uhuru jijini Maputo, Kiongozi huyo alieleza kwa hisia namna ambavyo ukombozi wa Msumbiji ulivyokuwa ni ushindi wa bara zima la Afrika – na kwa namna ya kipekee, Tanzania.

"Uhuru wa Msumbiji ni fahari yetu sote. Sisi ni ndugu wa damu; tulikuwa pamoja wakati wa mapambano, na leo tunaendelea kuwa pamoja katika kusherehekea matunda ya uhuru," alisema katika hotuba yake, akiweka wazi kuwa ukaribu wa mataifa hayo si wa kijiografia tu bali umetokana na historia ya pamoja ya mapambano ya ukombozi.

Katika hatua ya kutambua mchango wa waasisi wa mataifa hayo, aliwakumbuka kwa heshima kubwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Dkt. Eduardo Mondlane na Hayati Samora Machel, akieleza kuwa viongozi hao waliweka misingi imara ya mshikamano wa Afrika.

"Tanzania ilikuwa hifadhi salama ya wapigania uhuru wa Msumbiji. Iliruhusu mafunzo ya kijeshi, ilihifadhi wakimbizi, na ilitoa miundombinu ya kusaidia harakati za ukombozi – yote haya katika hali ya hatari na uchokozi wa moja kwa moja kutoka kwa wakoloni," alisema, akinukuu kauli ya shujaa Sergio Vieira kwamba "Tanzania ilifanya kitu cha kishujaa ambacho kisingeweza kufanywa na nchi nyingine yoyote."

Viongozi wa Msumbiji waliopata kuhudumu katika vipindi tofauti, akiwemo Rais wa sasa Daniel Chapo, walipewa pongezi kwa kuendeleza mafanikio ya taifa hilo tangu kupata uhuru wake mwaka 1975. Tanzania ilisisitiza uungaji wake mkono kwa Msumbiji katika hatua zinazofuata za maendeleo, hususan kupitia ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, ikitangaza mpango wa Shirika la Ndege la Tanzania kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Katika hotuba yake, Kiongozi huyo pia aliinua ajenda ya usawa wa kijinsia, akipongeza Msumbiji kwa kuifanya kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu: "Miaka 50: Kuwainua Wanawake, Kujenga Usawa wa Kijinsia." Alitambua mchango wa wanawake waliopigania uhuru kupitia Kikosi cha Wanawake cha FRELIMO, akiwataja mashujaa kama Josina Machel, Paulina Mateus Nkunda na wengine.

“Ukombozi wa wanawake si jambo la hisani,” alikazia, akinukuu maneno ya Samora Machel. “Ni msingi wa mapinduzi yenyewe.”

Katika kufunga hotuba yake, alitoa wito wa kuendeleza mshikamano wa kweli baina ya nchi za Afrika, akisisitiza kuwa baada ya mafanikio ya uhuru wa kisiasa, ni wakati sasa wa Afrika kulenga kwenye uhuru wa kiuchumi, maendeleo jumuishi, na umoja wa kitaifa.

"Leo kijiji kizima kimekuja kusherehekea na Msumbiji. Ushindi wenu ni wetu. Hatuna budi kuuenzi urithi huu kwa mshikamano, umoja na maendeleo ya pamoja ya Afrika yetu," alihitimisha.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad