Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuboresha miundombinu na huduma katika sekta ya usafiri wa anga nchini.
Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TCAA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. Akiwa kwenye ziara hiyo, alielezwa kwa kina kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na huduma za uongozaji ndege, usimamizi wa usalama wa anga, na fursa za mafunzo kupitia Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC).
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Kihenzile alieleza kufurahishwa kwake na hatua kubwa ambazo TCAA imefikia katika kuboresha huduma na mifumo ya usafiri wa anga. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono Mamlaka hiyo ili kuhakikisha Tanzania inajikita kuwa kitovu cha safari za anga katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Ubunifu, weledi na matumizi ya teknolojia ya kisasa ni nguzo muhimu katika kutoa huduma bora kwa wananchi," alisisitiza Mhe. Kihenzile.
Aidha, Kaimu meneja wa Kituo cha TCAA Dodoma Samuel Makalla alimueleza Naibu Waziri kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa, ikiwemo, mradi wa usimikaji wa rada nne za kisasa kwa ajili ya kuboresha ufuatiliaji wa ndege hewani; mfumo wa mawasiliano ya sauti kwa kutumia teknolojia ya VHF (Very High Frequency); mfumo wa kisasa wa usambazaji wa taarifa za anga (AIXM); na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Chuo cha Usafiri wa Anga.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yanafanyika chini ya kaulimbiu: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali Ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji,” yakishirikisha taasisi mbalimbali za umma. Taasisi hizo, ikiwemo TCAA, zinatumia jukwaa hilo kuonesha mafanikio, huduma na teknolojia mpya zinazotekelezwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu meneja wa Kituo cha TCAA Dodoma Samuel Makalla kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mamlaka hiyo pamoja na chuo cha usafiri wa anga (CATC) alipotembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akizungumza alipotembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akisaini kitabu katika banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akipokea zawadi kutoka kwa Kaimu meneja wa Kituo cha TCAA Dodoma Samuel Makalla aliyekabidhi kwa niaba ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment