HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 17, 2025

MWENYEKITI REB AIHAKIKISHIA USHIRIKIANO KAMPUNI YA KUZALISHA NA KUSAMBAZA UMEME YA MATEMBWE VILLAGE COMPANY YA MKOANI NJOMBE

-Inazalisha umeme wa kilowati 550 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kiyepa

-Inahudumia kaya 2,463 katika vijiji 8.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu ameihakikishia ushirikiano kampuni ya kuzalisha na kusambaza umeme ya Matembwe Village Company Limited ya Mkoani Njombe ili kuiwezesha kuongeza upatikanaji wa umeme na kuwafikia wananchi wengi zaidi waishio maeneo hayo.

Amethibitisha hayo alipofanya ziara katika mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa Matembwe uliopo katika Tarafa ya Lupembe Wilaya ya Njombe Mkoani Njombe Juni 17, 2025.

"Nimekagua mradi mzima kuanzia eneo la uzalishaji na nimetembelea baadhi ya wanufaika wa mradi ili kujionea uendeshaji wake, uwezo wake na namna ambavyo mradi huu unanufaisha wananchi katika kujiletea maendeleo," alifafanua Mhe. Balozi Kingu.

Alisema ameridhishwa na namna ambavyo mradi huo wa Matembwe unavyofanya kazi na alisisitiza kuwa ipo haja ya kuongeza uzalishaji hasa ikizingatiwa kuwa maji yapo yakutosha.

Aliuthibitishia uongozi wa mradi kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kutoa ushirikiano wa kuhakikisha uwezeshwaji unaendelea ili kuleta tija inayokusudiwa.

"Kazi iliyofanyika hapa ni kubwa na inaridhisha, ni wakati wenu sasa kujipanga vizuri kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme katika mradi huu ili walau mtoke kwenye kiwango mnachozalisha sasa cha kilowati 550 muweze kuzalisha umeme mwingi zaidi ili kuinua shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo haya na nchi nzima kwa ujumla ," alielekeza Mhe. Balozi Kingu.

Aliwasisitiza kuendelea kutunza mazingira ili kuwezesha miradi hii kuwa endelevu sambamba na kuwajengea uwezo vijana wa vijiji vinavyonufaika na mradi kwenye usimamizi na uendeshaji wa mradi.

"Vijana wanapaswa kutambua huu mradi ni wao; walianzisha babu zao na sasa wao wenyewe wananufaika," alisema.

Akizungumza hali ya uzalishaji na usambazaji umeme, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Matembwe, Johannes Kamonga alisema uhitaji wa umeme ni mkubwa hasa kipindi hiki ambacho viwanda vingi vinajengwa.

Aliipongeza REA kwa kuendelea kuuwezesha mradi huo na aliomba uwezeshaji uongezeke ili kuwezesha upanuzi wa mradi pamoja na kuunganisha wateja wengi zaidi

Alisema hapo awali mradi ulianza na kilowati 120 lakini kadri muda ulivyokwenda mahitaji yaliongezeka na hivyo walilazimika kutafuta uwezeshwaji ili kuongeza uzalishaji sambamba na kuongeza idadi ya wanufaika.

"Tunaishukuru REA kwani imekuwa bega kwa bega nasi, tulianza na vijiji viwili lakini kwa uwezeshwaji kutoka REA sasa tunahudumia vijiji nane," alisema Kamonga.

Akizungumzia uwezeshwaji wa mradi, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema REA imechangia takriban shilingi bilioni moja kuuwezesha mradi kuunganisha wateja 357 sawa na 16.18%.

Alisema REA imewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya kuzalisha na kusambaza umeme vijijini katika maeneo mbalimbali ndani ya mikoa yote Tanzania Bara ili kuwezesha wananchi wengi kufikiwa na huduma bora ya Nishati, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, kuongeza ajira nchini, kuongeza mapato serikalini na kuboresha maisha ya Watanzania waishio maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa mradi unatumia teknolojia ya kusambaza umeme kwa kutumia nyaya zinazopita ardhini suala ambalo alisema huongeza usalama na kupunguza gharama za matengenezo.

"Kwa sasa REA ipo katika hatua ya kuongeza idadi ya kaya 95 kupitia mkataba wa ruzuku ya nyongeza ya fedha," alifafanua Mha. Mwijage.

Mhandisi Mwijage alifafanua kuwa REA imefadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji nishati vijijini inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta Binafsi kwa kutoa ruzuku pamoja na kuwezesha mikopo ya masharti nafuu sambamba na kuwajengea uwezo waendelezaji wa miradi husika na miongoni mwa miradi iliyonufaika kwa Mkoa wa Njombe ni mradi huo wa Matembwe

Mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa Matembwe unaendeshwa na kusimamiwa na Kampuni ya Matembwe Village Company Ltd iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji vya Matembwe, Yembela na Ikondo.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad