Mkurugenzi wa Msama Production, Bw. Alex Msama, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anaongoza taifa hili kwa hekima na maono yanayoendana na muongozo wa Mungu. Alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Rais Samia unaakisi misingi ya kiroho, heshima kwa neno la Mungu, na dhamira ya kweli ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya haki na amani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Bw. Msama alisema, “Uongozi wa Rais Samia ni ushahidi wa dhahiri wa uwepo wa mkono wa Mungu katika taifa letu. Ameonyesha hekima, uvumilivu, na moyo wa upendo katika kuhudumia Watanzania wote bila ubaguzi.”
Msama alitoa mfano wa andiko la Biblia kutoka Warumi 13:2 linalosema: “Hivyo kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu.” Kwa mujibu wa Msama, andiko hili linathibitisha kuwa uongozi wa Rais Samia ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa taifa la Tanzania.
Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kumuunga mkono Rais Samia, kwani anatekeleza majukumu yake kwa unyenyekevu mkubwa, akijali maslahi ya wananchi, na kuweka mbele maadili ya uongozi wa kiroho.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kiongozi mwenye moyo wa utumishi kama Mama Samia. Ameendeleza miradi ya maendeleo, amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha amani, umoja, na mshikamano wa kitaifa. Haya ni matunda ya uongozi unaoongozwa na Mungu,” aliongeza Msama.
Mwisho, alitoa wito kwa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuendelea kumuombea Rais Samia na serikali yake, ili waendelee kusimama katika kweli, haki, na maono ya Mungu kwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment