HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 14, 2025

MHE MCHENGERWA AWATAKA MA RC, DC KUONGOZA JOGGING KWENYE MAENEO YAO


Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuwaongeza wananchi katika maeneo yao kufanya "jogging" na mazoezi ili kuimarisha afya.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Juni 14, 2025 mara baada ya kuongoza na kuhitimisha mbio za pole pole (jogging) za kilomita 10 zilizoratibiwa na Wizara yake katika eneo la Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma.

"Hamasa hii ya kufanya mazoezi iliasisiwa na viongozi wetu wakuu kuanzia enzi za Baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere hadi Rais wetu wa sasa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan lengo likiwa kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa nyemelezi hivyo na sisi tuna wajibu wa kuendelea kuwahamasisha watumishi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye " amefafanua Waziri Mchengerwa.
Aidha, amewataka watumishi wa TAMISEMI kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi wao pamoja na familia zao ili jamii yote iweze kuimarisha afya.

Amesema utamaduni wa kufanya mazoezi ukijengeka siyo tu kwamba utasaidia kuimarisha afya bali utasaidia kupunguza gharama za kutibu magonjwa ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na tabia bwete.

Pia Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania kuwa na tabia za kupima afya zao badala ya kungojea hadi wanapoumwa.

Mbio hizo za pole zilizohudhuriwa na mamia ya watumishi wa TAMISEMI ziliishia katika jengo la Ofisi ya TAMISEMI ambako kulikuwa na zoezi la upimaji wa afya kwa hiari.

Kwa upande mwingine, Mhe. Mchengerwa amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Wizara ya Elimu zinaratibu Mashindano ya Michezo kwa Shule za Msingi ( UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) ambapo amefafanua kuwa mashindano hayo yanasaidia kuibua vipaji vya wachezaji.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha mashindano hayo ili kuwajengea utamaduni wa wanafunzi kufanya mazoezi na kupenda michezo katika umri mdogo.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad