Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Watumishi mbalimbali wa Balozi wa Tanzania nchini Italia wakati akiwasili katika Ubalozi huo wakati akiwa ziarani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na mikutano mbalimbali ya uwili. Tarehe 23 Juni 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na baadhi ya watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia baada ya kuwasili katika Ubalozi huo akiwa ziarani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na mikutano mbalimbali ya uwili. Tarehe 23 Juni 2025.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasihi watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kuendelea kushirikiana na kuhakikisha wanaweka mkazo katika diplomasia ya uchumi na kulinda maslahi ya Tanzania katika uwakilishi wao.
Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia uliopo Jijini Roma akiwa ziarani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na mikutano mbalimbali ya uwili.
Makamu wa Rais amesema kuna fursa nyingi nchini Italia ambazo zitaweza kunufaisha pande zote mbili ikiwemo ushirikiano katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya Mifugo, TEHAMA, Viwanda na huduma za kijamii kama vile afya na elimu.
Amewasisitiza kuwavutia wawekezaji katika sekta ya utalii hususani ujenzi wa miundombinu ya utalii. Pia amesema Taifa limedhamiria kujikita katika kilimo janja hivyo ni vema kuvutia zaidi makampuni ya Italia ambayo yana uzoefu zaidi katika eneo hilo.
Amewataka kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania, kuendelea kuweka mkazo katika kutangaza Kiswahili na kuendelea kufundisha lugha hiyo kupitia utaratibu ulioanzishwa ubalozini hapo.
Amewasihi kuwasisitiza Watanzania waishio nchini Italia kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kutumia njia sahihi za uhamishaji fedha wakati wanafanya uwekezaji. Aidha ametoa rai kwa watanzania waishio Italia kufuata sheria za nchi hiyo pamoja na kujikita katika kufanya biashara halali zinazofuata taratibu na sheria za Italia.
Makamu wa Rais yupo nchini Italia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na mikutano mbalimbali ya uwili.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi pamoja, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Mkurugenzi Msidizi Idara ya Uwekezaji Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Fadhil Chilumba.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
23 Juni 2025
Roma - Italia
No comments:
Post a Comment