HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 27, 2025

Betty Mkwasa Aelezea Mchango wa TAMWA Katika Safari Yake ya Uongozi

 

MWANACHAMA mkongwe wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Betty Mkwasa, amepongeza mchango mkubwa wa TAMWA katika kumjengea ujasiri, umahiri na uongozi, ambao ulimwezesha kufanikisha mafanikio makubwa katika uandishi wa habari na katika nafasi za kiuongozi serikalini, ikiwemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wanachama wa TAMWA, Mkwasa amesema mafunzo aliyoyapata kupitia chama hicho ndiyo yaliyompa nguvu ya kupambana na changamoto za kijinsia na kielimu, hasa zinazowakabili wasichana na wanawake vijijini.

 "Nilipofika Korogwe, nilikuta wasichana wengi hawahudhurii shule na matokeo ya wanafunzi yalikuwa duni sana. Kupitia mafunzo na harakati nilizojifunza TAMWA, nilianzisha kampeni maalum kwa kushirikiana na wazazi na viongozi wa vijiji hadi wilaya kuhakikisha kila mtoto anayeruhusiwa kisheria kuwa shuleni anarudi shuleni," amesema Mkwasa.

Kwa jitihada hizo, anasema aliweza kuwarudisha zaidi ya watoto 400 waliokuwa wameacha shule na kujihusisha na shughuli mbalimbali, hali aliyosema ilitokana na malezi ya TAMWA.

Baada ya mafanikio hayo Korogwe, Mkwasa alihamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, ambako alikuta hali ya elimu kwa mtoto wa kike ikiwa duni mno, kiasi kwamba haikuwa kawaida kwa mtoto wa kike kufika kidato cha tano.

 "Kwa kutumia maarifa niliyojifunza TAMWA, niliwapa mafunzo madiwani wanawake wa viti maalum. Tulitembea kata kwa kata tukiwaelimisha wasichana kuhusu umuhimu wa elimu na nafasi yao katika maamuzi ya kitaifa," amesema.

Mafanikio ya kampeni hiyo yaliwafanya kuanzisha vilabu vya wanafunzi shuleni, wakitunga katiba na sheria ndogondogo zilizowasimamia kuhakikisha wasichana wanasoma kwa bidii na kushiriki katika maamuzi ya shule.

 "Leo najivunia kuona Wilaya ya Bahi kwa mara ya kwanza imefanikiwa kuwapeleka watoto wa kike 45 kidato cha tano. Hii ni kutokana na maarifa niliyopewa na TAMWA," ameongeza kwa fahari.

Betty Mkwasa ni mfano hai wa jinsi taasisi kama TAMWA zinavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake katika uandishi wa habari, uongozi na harakati za kijamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad