• Airtel, UNICEF wagawa vifaa vya intaneti ya kasi Kuimarisha Elimu ya Kidijitali Dodoma
• Airtel UNICEF waunganisha shule 30 Mkoani Dodoma na intaneti ya BURE
Kampuni ya Airtel Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia mradi wake wa kijamii wa Airtel SmartWASOMI, imekabidhi na kufunga vifaa vya intaneti ya kasi kwa shule 30 za sekondari mkoani Dodoma. Vifaa hivi vitawawezesha walimu na wanafunzi kupata huduma ya intaneti bure, ili kujisomea bure kupitia maktaba mtandaoni ya Taasisi ya Elimu Tanzania na majukwaa ya elimu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mtemi Mazengo, Mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kanda ya Airtel Tanzania Dodoma, Bw. Salum Ngururu alisema, SmartWASOMI siyo tu mtandao, bali ni mfumo wa kidijitali unaoleta vifaa, maudhui ya kielimu yanayolingana na mtaala, na jukwaa la usomaji na ufundishaji wa kisasa
“Mpango huu unaunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano katika kutumia teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA) kwenye sekta ya elimu,” alisema meneja huyo.
Naye Bi. Grace Samwel akizungumza wa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma,aliishukuru Airtel na kusema, “Shule zetu sasa zinaweza kusoma kidijitali kwenye maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu (TET) au kupata maudhui kutoka maktaba mtandao ya Shule Direct bila bila gharama ya bando, tunawashukuru Airtel kwa kuwezesha elimu ya kidijitali kufika hadi kwa wanafunzi wetu bila gharama yoyote.”
Pia Airtel imeeleza kuwa mradi wa Airtel SmartWASOMI tayari umeshatekelezwa katika mikoa ya Zanzibar, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mbeya na sasa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuunganisha shule 3,000 nchini kwa kushirikiana na Serikali na UNICEF.
Kwa upande wake, Mwalimu Florian Kashasila alisema; “Vifaa vya intaneti ya kasi ya Airtel tulivyopatiwa leo vitasaidia sana walimu na wanafunzi kupata nyenzo za kufundishia na kujifunzia, ambazo awali hazikupatikana kirahisi shuleni.”
Airtel Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa sehemu ya mabadiliko ya elimu nchini kwa kuhakikisha shule haziachwi nyuma katika safari ya ujumuishaji wa kidijitali.
Afisa wa Kitengo cha Ufundi wa Airtel Tanzania, Bw. Harrison Isdory (aliyesimama), akitoa maelezo kwa wakuu wa shule za sekondari mkoani Dodoma kuhusu mradi wa Airtel SmartWASOMI na jinsi vifaa vya intaneti vya Airtel Tanzania vitakavyoboresha ufundishaji na usomaji kwa njia ya kidijitali katika shule za sekondari mkoani humo. Kushoto ni Meneja wa Kanda wa Biashara wa Dodoma wa Airtel Tanzania, Bw. Salum Ngururu, na upande wa kulia ni, Mwakilishi wa Afisa Elimu Sekondari wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Grace Samweli.
Mwakilishi wa Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Dodoma, Bi. Grace Samweli, (kushoto) akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pandambili, Bw. Mengi Lekuchela, vifaa vya intaneti vya Airtel Tanzania wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa zaidi ya 30 kwa ajili ya shule za sekondari iliyofanyika mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki. Msaada wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Airtel SmartWASOMI ili kurahisisha upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kusomea kidijitali bila gharama yoyote kwa shule zote za sekondari nchini.
Mwakilishi wa Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Dodoma, Bi. Grace Samweli (Kulia), Meneja Biashara wa Kanda wa Airtel Tanzania, Salum Ngururu (kushoto) na Afisa wa Kitengo cha Ufundi wa Airtel Tanzania, Bw. Harrison Isdory (Katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa shule za sekondari jijini Dodoma, mara baada ya makabidhiano ya vifaa vya Intaneti chini ya mpango wa Airtel SmartWASOMI. Msaada wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Airtel SmartWASOMI ili kurahisisha upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kusomea kidijitali bila gharama yoyote kwa shule zote za sekondari nchini.
No comments:
Post a Comment