HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 30, 2025

WAZIRI KOMBO AWASISITIZA MACHIFU KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasisitiza Machifu wa Kanda ya Vita ya Majimaji Kusini mwa Tanzania kuendelea kushirikiana na Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao ya kimila katika jamii.

Hayo yamejiri wakati Waziri Kombo alipokutana na ujumbe huo wa machifu katika ofisi za Wizara jijini Dodoma na kuzungumza nao masuala mbalimbali ya kimkakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Utamaduni.

Wakieleza lengo la ujio wao, Machifu hao wameeleza kiu ya kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha nchi inakuwa na utulivu na amani hususan katika maeneo ya mipakani kupitia ushirikiano walionao na machifu wa nchi jirani ili kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru ya kueleta amani nje ya mipaka na kuisisitiza jamii kuifanyia kazi falsafa hiyo muhimu.

Pia, wameeleza maeneo yenye tija katika ushirikiano wa machifu hao na machifu wa nchi jirani ni pamoja na kupeana taarifa za tahadhari na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi wao ikiwemo; taarifa za biashara haramu, kusaidia operesheni za amani na ulinzi, utunzaji wa mazingira, tahadhali za ukame na ukosefu wa chakula na kukuza matumizi ya lugha ya kiswahili.

Kadhalika, wameeleza kuwa wanatarajia kuwa na tamasha la Chief Hangaya Mtembele Festival linalotarajiwa kufanyika mkoani Mtwara ambalo litatumika kutangaza fursa mbalimbali za utalii na historia ya utamaduni katika ukanda huo wa kusini. Tamasha hilo litashirikisha kabila la wayao kutoka katika nchi za kusini mwa Afrika za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe na Malawi.

Wamesema tamasha hilo muhimu litasaidia kushirikishana na kupeana uzoefu katika masuala mbalimbali yatakayosaidia kuenzi misingi ya utamaduni ambayo inafafanana kati ya Tanzania na nchi jirani. Wameeleza kuwa katika majukumu yao wamekuwa wakisimamia amani na uadilifu katika jamii, kuisisitiza jamii kuzingatia sheria, kanununi na taratibu za nchi na madhara ya utandawazi katika utamaduni wa muafrika.

‘’Historia ya nchi yetu ina thamani kubwa kwa historia ya nchi yetu vizazi vyetu na hii inahususha historia ya mkoloni tangu enzi za utawala wa Mjerumani katika ukanda wa Vita ya Majimaji ambapo jamii hiyo ilipigana vita ya Majimaji na Mjerumani hadi wakati wa harakati za kuikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla dhidi ya udhalimu wa mkoloni zilizoongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere’’ alieleza Chifu Zulu Gama.

Naye Waziri Kombo amewahakikishia machifu hao kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na kwamba watambue kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameupa umuhimu mkubwa umoja wa machifu nchini na kila mwaka amekuwa akishiriki tamasha la machifu ili kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za machifu nchini.

‘’Nikiwa Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nilifanikisha kutungwa kwa sheria ya tiba asilia iliyofanikisha kuanzishwa kwa kitengo maalum cha tiba asilia’’ alieleza Waziri Kombo.

Hivyo, akasisitiza ni vema uongozi wa machifu kitaifa ukawa na takwimu sahihi ya idadi ya machifu waliosajiliwa pamoja na katiba ya kuwatambulisha kimataifa ili kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika kutekeleza na kufanikisha malengo yao.

Pia akasisitiza Jumuiya za kikanda kama vile Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (IGCLR) na Jumuiya za Kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa (UN) zinatambua nafasi ya machifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba Wizara itashirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni Wizara Mama inayosimamia machifu katika kuwajengea uwezo wa masuala ya kimataifa na namna ya kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana duniani.

Waziri Kombo amewasihi machifu hao kuwaeleza wananchi katika maeneo yao juu ya fursa mbalimbali zinazoratibiwa na Wizara ikiwemo ajira 1,000 zilizotolewa na Serikali ya Qatar na ajira 10,000 zinazotarajiwa kutolewa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) kwa vijana wa Tanzania. Vilevile, ameahidi kuzungumza na Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje kutoka katika nchi za Kusini mwa Afrika ili kuendelea kufungua fursa za ushirikiano kati ya machifu wa kanda ya Vita ya Majimaji Kusini mwa Tanzania na machifu wa nchi za kusini mwa Afrika.











No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad